Wakati wa ziara rasmi ya Rais Daniel Chapo mjini Kigali, mataifa hayo mawili yamefikia makubaliano ya amani na usalama ambayo yanatazamiwa kuimarisha ushirikiano wao katika kukabiliana na changamoto za kiusalama.

Rwanda na Msumbiji zimetia saini makubaliano ya “amani na usalama” wakati wa ziara ya rais Daniel Chapo mjini Kigali nchini Rwanda.

Vikosi vya nchi hizo mbili vinapambana na uasi wa muda mrefu wa makundi ya itikadi kali katika Jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji. Rais Paul Kagame amepongeza hatua hiyo na amesisitiza mahusiano madhubuti kati ya mataifa hayo mawili. 

Hii imekuwa ni ziara ya kwanza ya kikazi ambayo Rais mpya wa Msumbiji Danaiel Chapo ameifanya nchini Rwanda tangu alipochukua madaraka Januari 15 mwaka huu.

Katika ziara hii ya siku tatu marais hao wawili wameongoza zoezi la kutia saini mikabata miwili ya amani na usalama pamoja na biashara na uwekezaji. Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa na pande mbili kuhusu undani wa mkataba huu wa amani na usalama, alibainisha msemaji wa jeshi la Rwanda kwa shirika la habari la AFP.