Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wimbi kubwa la watu kuamua kujitoa uhai lililoikumba jamii katika siku za hivi karibuni linadaiwa kutosababishwa na matatizo ya afya ya akili; JAMHURI linaripoti.

Utafiti wa Hospitali ya Afya ya Akili ya Milembe iliyopo jijini Dodoma na wa wataalamu mbalimbali wa afya umeonyesha kuwapo kwa wimbi hilo sambamba na vifo vya ghafla na kuvihusisha na matatizo ya afya ya akili.

Hata hivyo, mtaalamu wa magonjwa ya akili wa Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, Dk. Jovina Joseph, anasema uamuzi wa watu kujitoa uhai hausababishwi na afya ya akili.

Akizungumza na JAMHURI wiki iliyopita, Dk. Jovina anasema hali hiyo ni matokeo ya changamoto mbalimbali ambazo mtu hukakabiliana nazo (akilini).

“Kwa binadamu msongo wa mawazo ndiyo sababu kuu inayofanya mtu kujiua,” anasema.

Hiyo ni mbali na mtu kupata mshtuko (au presha) unaoweza kumsababishia kifo.

Anasema watu wengi huamua kujiua kutokana na changamoto kadhaa za maisha kama vile hofu ya kufilisiwa kutokana na mikopo kutoka taasisi za fedha au watu binafsi inayofahamika kama ‘kausha damu’.

Anataja hofu ya kutekwa na matatizo ya ukatili wa kijinsia au uhusiano mbovu katika familia kuwa ni sababu nyingine za ongezeko la watu kujiua.

“Tatizo lililopo ni kwamba wengi hukosa msaada wa kisaikolojia hasa wanapokutana na changamoto nyingi au kubwa wanaazoshindwa kuzistahimili, badala yake hufanya uamuzi wa haraka.

“Hakuna afya ya akili inayosababisha kujiua ghafla, bali ni mkusanyiko wa changamoto zinazosababisha hasira. Mtu anajiua kwa sababu ya changamoto za afya ya akili na kujiondoa kwake ni kwa sababu ameshindwa kupata msaada wa haraka.

“Ukiona mtu amejiondoa uhai, usidhani kuwa alikumbana na tatizo hilo siku hiyo hiyo, Hapana. Ukifuatilia historia yake, utakuta ameishi nalo kwa muda mrefu, kisha akapata tukio jingine la ghafla,” anasema Dk. Jovina.

Kwa utafiti wake, Dk. Jovina, anasema asilimia kubwa ya watu hujiua kwa sababu ya kufilisiwa kutokana na mikopo au kukabiliwa na matatizo ya mrundikano wa kodi za serikali.

Anasema mtu akipatwa na hali hii hujisikia kama vile amepoteza kila kitu, hivyo uamuzi wa mwisho kwake ni kujiua.

“Ushauri wangu kwa watu ni kuacha ‘panic’ (hofu/wasiwasi) ya haraka kwa sababu maisha ya binadamu katika hali hiyo ni hatari sana, inaweza kusababisha madhara makubwa hata kifo.

“Kuna mfano halisi wa mtu mmoja aliyejulishwa kuwa mali zake zimeibwa; akapata mshtuko, akaanza kutapika damu. Baada ya saa mbili, akapa presha na mwishowe akafariki dunia,” anasema.

Dk. Jovina anasema mara kadhaa watu wanaojiua katika uhusiano hukabiliwa na changamoto zinazofanana na kudumu kwa muda mrefu bila kutatuliwa na wahusika wawili au jamii.

Anasema katika hatua hiyo utaona ndugu wanaweza kuhusika kujaribu kusuluhisha lakini hakuna suluhu inayofaa,  hali hii inasababisha mtu kuona hakuna njia nyingine zaidi ya kujiondoa uhai.

“Mara nyingi watu wa aina hii hukosa ushauri wa kisaikolojia mapema, si kwamba ni jambo la ghafla, bali ni matokeo ya mrundikano wa changamoto kichwani,” anasema.

Awali Taasisi ya Tiba kwa Ushauri ya Hospitali ya Mirembe jijini Dodoma, ilidai kwamba kiwango cha watu kufariki dunia ghafla kinaongezeka kwa kasi ya kutisha.

Wataalamu wanasema watu wengi wanaojiua hupitia vipindi vya mfadhaiko, kuchanganyikiwa, hofu na msongo wa mawazo.

“Sababu hizi zote huongeza hatari ya shinikizo la damu, ambayo pia husababisha kushindwa kwa moyo au kiharusi, na bila shaka husababisha kifo cha ghafla, ambacho sasa ni (kitu) cha kawaida,” inasema taasisi hiyo.

Milembe imetoa tafadhali ya watu kuepuka kukasirishwa kirahisi na watoto, marafiki, wafanyakazi wenzao, wakubwa wao, wasaidizi, wapenzi, waume na wake zao na kuwataka watu kujitenga na usumbufu.