Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umeanza jijini Pretoria, Afrika Kusini Machi 07, 2026, chini ya Uenyekiti wa Balozi Tebogo Seokolo ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano ya Afrika Kusini.
Katika hotuba ya ufunguzi Balozi Seokolo alihimiza Nchi Wanachama kuchukua hatua za kukuza zaidi mtangamano wa Kikanda kwa kuongeza kiwango cha Biashara baina ya Nchi za SADC kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 23.

Kwenye hotuba hiyo alihimiza umuhimu wa Nchi Wanachama kuimarisha sekta za Viwanda, kwa kuzingatia kwamba sekta hiyo inakua kwa kasi na inachangia asilimia 11 ya pato la ndani (GDP) la nchi za SADC.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu haswa barabara ili kurahisisha mwingiliano na mtangamano wa watu na biashara ndani ya Kanda; na usalama wa chakula na lishe, haswa ikizingatiwa kuwa watu milioni 58 katika kanda ya SADC wana changamoto ya usalama wa chakula.
Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa alieleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha maeneo hayo kwa kushirikiana na Nchi Wanachama wa SADC.








