
Na Kulwa Karedia , Jamhuri Media,Unguja
Mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na mgombea ubunge Jimbo la Donge, Sadifa Juma Khamis, amesema wagombea urais wa Chama Cha Mapinduzi,(CCM) Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein Mwinyi wanapaswa kuendelea kuongoza kwa miaka isiyopungua 20.
Amesema hatua hiyo inatokana na mafanikio makubwa ya maendeleo waliofanya Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita .
Akizungumza wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja Septemba 18,2025,Sadifa aliwaomba wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuwapigia kura za ndiyo viongozi ili warudi kukamilisha ndoto zao.
Amesema taifa linahitaji kuendeleza kasi ya maendeleo inayoonekana katika sekta mbalimbali.
“Wagombea tuliokuwa nao wanatosha, na mimi nikiwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nawaambia hawa viongozi wanafaa kuendelea kwa miaka isiyopungua 20,”amesema.

Sadifa amesema hakuna upinzani wa kweli ndani ya Jimbo la Donge wala Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, akisisitiza kuwa wapinzani wameishiwa hoja mbele ya utekelezaji bora wa ilani ya CCM.
“Nikuhakikishie, Jimbo la Donge sisi tumemaliza hakuna upinzani. Zanzibar hakuna anayempinga Dkt. Mwinyi, na Tanzania hakuna wa kumtisha Mama Samia Suluhu Hassan,”amesema.
Kuhusu miradi ya maendeleo, Sadifa alitaja mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya barabara, afya na miundombinu kama msingi wa uungwaji mkono kwa CCM.
“Leo ukienda Wilaya ya Kati, barabara tisa zimejengwa. Bodaboda wanasema wanatoa kura za ndiyo. Kuna hospitali za kisasa kama hoteli za nyota tano. Hili ni jambo la kujivunia,” amesema.
Katika kukoleza hoja yake, hakusita kusimulia tukio la mzungu aliyepotea njia akiwa njiani kuelekea hotelini na kujikuta kwenye soko la Chuwini, akidhani ni hotelini.

“Mzungu alijua anaenda hotelini, kumbe alikuwa anaenda sokoni maana hata masoko sasa yanaonekana ya kisasa,” alisema kwa utani.
Amesema ushindi wa CCM katika uchaguzi ujao hauna shaka, na kwamba hata baadhi ya wapinzani wamekuwa wakionesha kuunga mkono maendeleo yanayotekelezwa na serikali ya CCM.
Amesema kwa mwelekeo huo wagombea wote wa chama hicho hawapaswi kuwa na hofu ya ushindi.

