Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dubai umerejesha huduma zake leo baada ya kufungwa kwa muda kufuatia moto uliotokea katika tanki la mafuta uliosababishwa na shambulizi la droni.

Tukio la kuwaka moto kwa tanki la mafuta, ambalo halikusababisha majeruhi, ni shambulizi la tatu kulenga uwanja wa ndege wa Dubai tangu Iran ilipoanzisha mashambulizi ya kisasi dhidi ya mataifa ya Ghuba tarehe 28 Februari. Iran inasema mashambulizi hayo yanalenga uwepo wa Marekani katika kanda hiyo.

Aidha, shambulizi jingine la droni limeripotiwa kulenga miundombinu ya mafuta katika pwani ya mashariki ya Umoja wa Falme za Kiarabu. Kwa mujibu wa mamlaka za nchi hiyo, shambulizi hilo lilitokea katika eneo la uzalishaji wa mafuta la Fujairah na kusababisha moto mkubwa, huku juhudi za kuudhibiti zikiendelea.

Eneo hilo liko katika pwani ya UAE kwenye Ghuba ya Oman, nje ya Mlango Bahari wa Hormuz, ambao kimsingi umefungwa na Iran. Saudi Arabia pia imesema imezuia wimbi la droni za Iran zipatazo 35 zilizorushwa kuelekea mkoa wake wa mashariki wenye visima vikubwa vya mafuta.