Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Mhitimu wa Shahada ya Umahiri ya Mawasiliano ya Umma katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Ahmed Sagaff amechukua na kurejesha fomu ya kuomba ridhaa kuteuliwa kuwania ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi katika Jimbo la Dodoma Mjini kwenye uchaguzi mkuu 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini hapa mara baada ya kurejesha fomu hiyo Sagaff amesema amechukua uamuzi huo kwa kuwa anaamini anaweza kusimamia utekelezaji wa ahadi zilizopo kwenye Ilani ya uchaguzi ya CCM 2025-2030 katika jimbo hilo ili kuunga mkono jitihada za serikali za kustawisha maisha ya wakazi wa Dodoma Mjini na Watanzania wote kwa ujumla.
“Nakwenda kuomba ridhaa ya kuendeleza mema yaliyofanywa na Ndg. Anthony Mavunde, nitaomba idhini ya kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika kutimiza maono yake, na nitaomba ruhusa ya kuwawakilisha kikamilifu wakazi wa Dodoma Mjini,” ameahidi.
Kabla ya kuingia rasmi kwenye siasa, Sagaff amehudumu kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda wa miaka mitano (2020-2025) kama Afisa Habari akiwa na majukumu ya kufuatilia na kutangaza utekelezaji wa miradi, programu, sera, na mipango ya serikali.
“Katika utumishi wa umma nimejifunza namna serikali inavyopunguza umasikini, inavyoimarisha usawa wa kijinsia, na mengine mengi, kikubwa zaidi nimejifunza kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi,” amedokeza.
Kitaaluma, Sagaff ni mwanahabari aliyepata elimu yake katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Chuo Kikuu Tumaini (TUDARCo), na Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar (ZJMMC).
“Mwenyezi Mungu anasema kwamba elimu tuliyopewa wanadamu ni ndogo sana, hivyo hatupaswi kujikweza bali tunapaswa kuzitumia elimu zetu katika kuwatumikia wanadamu wote na kuhakikisha kwamba dunia inaendelea kuwa sehemu salama ya kuishi,” ameeleza.
