Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, amesema kuwa huduma ya msaada wa kisheria ni muhimu kwa Watanzania na Wizara yake inafanya jitihada kuhakikisha huduma hiyo inakuwa endelevu kwa manufaa ya wananchi.

Akizungumza jana Julai 8, 2025, wakati alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Saba Saba, Sagini alisema kuwa tayari Wizara imeanza kupeleka maofisa wake katika ngazi ya Halmashauri ili kuwasaidia wananchi kwa kuwapatia msaada wa kisheria katika maeneo yao.

“Maeneo tutakayoyapa kipaumbele ni elimu kwa umma. Tumegundua kuwa malalamiko mengi yanatokana na ukosefu wa elimu stahiki, hasa katika sekta ya umiliki wa ardhi,” alisema Sagini.

Aliongeza kuwa Wizara imeweka mkazo kwa maafisa na wasajili wa ardhi waliopo katika ngazi ya Mkoa kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu haki na taratibu za umiliki wa ardhi.

“Tumewapa changamoto maafisa wetu wawape wananchi elimu ya ardhi ili kupunguza malalamiko yasiyo ya lazima. Tukifanya hivyo tutakuwa tumejenga msingi mzuri wa utoaji haki,” alifafanua.

Naibu Waziri Sagini aliipongeza pia serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa yanayofanyika katika sekta ya sheria na utoaji haki nchini, huku akisisitiza kuwa jitihada hizo zimeanza kuleta matokeo chanya.

Aidha, alitumia fursa hiyo kulisifu banda la Wizara ya Katiba na Sheria kwa ubora wake na huduma bora zinazotolewa, na kufichua kuwa banda hilo limetangazwa kuwa mshindi wa jumla namba moja miongoni mwa taasisi za serikali.

“Hongereni watu wa Katiba na Sheria kwa mapokezi bora. Kila mtu anayefika anapokelewa vizuri na kupewa elimu na wataalamu. Wengi niliowaona waliridhishwa na huduma,” alisema.

Pia aliwataka wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea banda hilo ili kujifunza masuala mbalimbali ya kisheria yanayohusu maisha yao ya kila siku.

Katika hatua nyingine, Sagini alitembelea banda la Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambapo alieleza kufurahishwa na namna wananchi walivyojitokeza kwa wingi kuomba vyeti vya kuzaliwa.

Hata hivyo, alieleza kusikitishwa na hali ya wananchi wengi kukosa taarifa kwamba huduma hizo zinapatikana hadi ngazi ya wilaya na si lazima kusubiri maonesho kama haya.

“Hakuna sababu ya watu kusubiri Saba Saba ndipo waje kwa wingi kufuatilia vyeti vya kuzaliwa, kwani huduma hizi zipo hata wilayani. Wanafika hapa wakikuta vyeti vimeshapelekwa huko huko walikotoka,” aliongeza.