Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kufanya mageuzi ya kodi mbalimbali endapo wananchi watampa ridhaa ya kuongoza tena nchi.
Amesema tume ya kukosa maoni kuhusu masuala ya kodi imekamilisha mchakato wake.
Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, wakati wa mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu zilizofanyika uwanja wa Cheka leo Oktoba 22,2025.
Tumeunda tume ya kukusanya maoni kuhusu masusla ya kodi, nashukuru imemaliza kazi yake wakati tunaingia kipindi cha kampeni, wataleta taarifa yao baada ya kuunda serikali mkitupa ridhaa yenu, tutafanya mageuzi ya kodi zetu,lengo kubwa ni kuona kodi zetu zinakuwa rafiki kwa kila,amesema
Amesema tume nyingine ambayo aliiunda ni ile ya kuangalia Haki Jinai kwenda kuangalia masuala ya haki, hazi za watu zinaamuliwa, zinapatikana vipi na wanafanya vipi.
Wote mnajua tume ile ilimaliza kazi yake ikatuletea taarifa, sasa sekta yetu ya haki, mahakama zetu na sheria ziko vizuri sana, sasa, haki za watu hazipotei kama zilivyokuwa, hazicheleweshwi kama hapo nyuma, sasa hivi polisi,mahakama, mwendesha mashtaka wa serikali, DCI wote wanasoma, linaloandikwa leo polisi wanasomana kwenye mitandao.
Sasa hivi haki ya watu inapatikana, tunaendelea kujenga miundombinu ya mahakama za wilaya, mikoa, mahakamu za hakimu mkazi tunaendelea kujenga,amesema.
Amesema tume ya tatu aliyounda ilishughulikia uhusiano wa nje kwa sababu miaka kadhaa iliyopita hakukuwa na uhusiano mzuri katika eneo hilo.
Uhusiano wetu na mambo ya nje tulifika mahali mambo yakawa siyo mazuri sana, wakafanya kazi, wametuletea sasa tumeweza kurudisha heshima kwenye mataifa ya nje, Tanzania inaheshimika sana na tunategemewa sana,amesema.
Amesema tume nyingine iliyoundwa ilikuwa ile ya kutengeneza dira baada ya kumaliza Dira ya Taifa ya miaka 25, lazima tuwe na dira nyingine ambayo inatupeleka miaka mingi kama hiyo.
Tume hii iliongozwa na Dk Asga Rose Migiro, tumepata dira yetu Tanzania sasa kila tunachokipanga tunaangalia humo,amesema
Amesema aliunda pia tume ya kuangalia mgogoro wa eneo la Liliondo nayo imekamilisha kazi yake, hivyo wanatarajia kuwasilisha baada ya kuunda serikali
Wamemaliza kazi yao, wataleta maoni yao na tutachukua hatua stahiki baada ya kuunda serikali, nataka kuwaambia tume zote hizi na zile ambazo zimesahau kuzitaja hapa zimekwenda kwa wananchi kuwasilikiza na kuchukua maoni yao, huu ndiyo utawala bora hakuna mtu anayejua kila kitu.
Mkitaka kuendesha nchi kwa amani, lazima uwashirikishe wenye nchi na ndiyo demokrasia, tunafanya kazi kwa ajili ya watu na wao ndiye wenye msingi wa wa kuendesha nchi hii si watawala,amesema.
Amesema katika utawala, wamejitahidi kuboresha majengo mbalimbali ya serikali ambayo yanatoa huduma kwa wananchi sasa yanaweza kupokea hata watu wenye ulemavu, wamejengea majengo 127 katika halmashauri mbalimbali.
