Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Mkoa wa Tabora umetumia zaidi ya shilingi trilioni 15 kutekeleza miradi ya kimkakati katika sekta mbalimbali, tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani mwaka 2021 chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Matiko Chacha,amesema hayo leo Julai 11,2025 Jijini hapa wakati akizungumzia mafanikio ya serikali ya awamu ya Sita na kueleza kuwa fedha hizo zimewezesha mkoa huo kupiga hatua kiuchumi, kijamii na kiutawala, ambapo pato la mkoa limekua kutoka trilioni 5.4 mwaka 2020 hadi trilioni 6.3 mwaka 2024, huku pato la mtu mmoja mmoja likiongezeka kwa asilimia 4.5.

Katika sekta ya afya amesema, hospitali tano za wilaya zimekamilika, vituo vya afya 30 vimejengwa, na zahanati 109 zimekamilishwa huku upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umeongezeka hadi asilimia 91, ikiwa ni matokeo ya ongezeko la bajeti kutoka shilingi bilioni 4.2 hadi bilioni 9.8 ndani ya kipindi hicho.

“Sekta ya elimu imeimarishwa kupitia mpango wa elimu bila malipo, ambapo shule za msingi zimeongezeka kutoka 819 hadi 990 na shule za sekondari kutoka 197 hadi 264,Serikali imetoa zaidi ya bilioni 146.6 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu na kuongeza ufaulu wa wanafunzi, “amesema

Kwa upande wa miundombinu, Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora ameeleza kiwa barabara za lami zimeongezeka, madaraja 116 yamejengwa, na taa za barabarani zimeongezeka kutoka 550 hadi 1,850.

Pia, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaendelea sambamba na ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Tabora kwa zaidi ya shilingi bilioni 24.

Katika sekta ya kilimo na mifugo,ameeleza kuwa eneo la umwagiliaji limeongezeka hadi ekari 37,560, na uzalishaji wa tumbaku umeongezeka kutoka kilo milioni 29 hadi milioni 62. Zaidi ya majosho 95 yamejengwa kwa ajili ya mifugo na huduma za ugani zimeimarishwa kwa vifaa na usafiri.

“Huduma za maji mijini na vijijini zimeboreshwa ambapo upatikanaji wa maji umeongezeka hadi asilimia 89.1 mijini na asilimia 68.2 vijijini,Miradi 73 ya maji imekamilika vijijini huku mabwawa ya maji yakiimarika kutoka 10 hadi 13 maendeleo haya ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuboresha maisha ya Watanzania wote, “amesisitiza