……927 wapimwa saratani

Na Mwanandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marko, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wa pembezoni kupitia Kampeni ya Huduma za Mkoba za uchunguzi wa saratani zinazoendeshwa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI).

Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo ya siku tatu katika Hospitali ya Wilaya ya Serengeti, Angelina alisema huduma hizo zimetoa fursa kubwa kwa wananchi kutambua afya zao kwa wakati.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia kwa kutuwezesha kupata huduma hizi muhimu hapa Serengeti. Serikali inaendelea kuokoa maisha kwa kuhakikisha wananchi wa vijijini hawakosi huduma za kibingwa,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Aidha, alisisitiza kuwa Serikali ya Wilaya itahakikisha wananchi wote waliopata rufaa wanafika Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

“Hakuna mgonjwa wa Serengeti atakayekosa kufika Ocean Road kwa sababu ya kutokuwa na nauli. Tutahakikisha tunaokoa maisha ya wananchi wetu,” alisisitiza.

Naye Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti, Johanece Bakuba, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Wilaya, aliushukuru uongozi wa serikali na ORCI kwa kutekeleza kambi hiyo kwa mafanikio.

“Baada ya kambi hii, tutaendelea na kambi nyingine Januari hapa hapa Serengeti. Tunawaomba wananchi mkipata taarifa za kambi ya uchunguzi basi muweze kuhamasishana kwa ajili ya uchunguzi wa mapema,” alisema Bakuba.

Katika hatua nyingine, Daktari Bingwa wa Saratani na Mkurungezi wa huduma za kinga wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Crispin Kahesa, alitoa takwimu rasmi za matokeo ya kambi hizo mbili za uchunguzi wa saratani.

“Jumla ya wananchi 927 walihudumiwa katika wilaya za Bukombe na Serengeti. Kati yao, 27 walibainika kuwa na viashiria vya saratani na tayari 41 wameanza matibabu ya awali. Tulichukua sampuli mbili kwa uchunguzi wa kitaalamu zaidi na wagonjwa watatu wamepewa rufaa kwenda ORCI kwa matibabu zaidi,” alisema Dkt. Kahesa.

Dkt. Kahesa aliendelea kwa kutoa takwimu kwa kila wilaya ambapo wilaya ya Bukombe wananchi 379 walipimwa na tisa walionekana na dalili za awali za saratani na walipewa matibabu huku watatu wakipewa rufaa.

Kwa upande wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara alisema wananchi 548 walipimwa na 18 walionekana na dalili za awali za saratani na walipewa matibabu na wawili walipewa rufaa.

“Matibabu ya saratani ni gharama. Ndiyo maana ORCI inatoa matibabu kulingana na uwezo wa mgonjwa. Muhimu ni kufika mapema ili tuokoe maisha,” alisisitiza Dkt. Maguha.

Wananchi pia walipata elimu ya saratani kupitia Balozi wa Saratani Tanzania, Cedou Mandigo “Babu wa Kitaa”, ambaye aliwahi kuungua ugonjwa wa saratani na kutibiwa na taasisi ya saratani Ocean Road na kupona, ambapo aliwahimiza wasikate tamaa wanapopata majibu chanya.

“Saratani ikigundulika mapema inatibika. Tusisubiri hadi hali iwe mbaya,” alisema Mandigo.

Kambi hizi zimeonyesha dhamira ya serikali kupambana na saratani kwa kufikisha huduma za kibingwa hadi ngazi ya jamii. Kauli Mbiu ya kambi hii ni “Fanya Uchunguzi — Okoa Maisha.”