Na Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Katika hali ya hewa nzuri ya Jiji la Dodoma, asubuhi ya Agosti 27, 2027, historia imeandikwa tena pale Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipowasili katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Njedengwa, kurejesha rasmi fomu ya kugombea nafasi ya urais kwa muhula wa pili kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi, pamoja na viongozi waandamizi wa chama hicho, Dkt. Samia amekabidhiwa fomu hiyo na Mkurugenzi wa INEC, Kailima Ramadhan, na kukamilisha hatua muhimu inayoweka msingi wa safari mpya ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Tofauti na mwaka 2020, ambapo aligombea kama mgombea mwenza, safari hii Dkt. Samia anarejea uwanjani akiwa tayari na rekodi ya utendaji, sura ya matumaini, na kauli mbiu ya utulivu, umoja, na maendeleo jumuishi.
Hatua ya kurejesha fomu hii haikuwa tu ishara ya nia ya kuendelea kuongoza taifa, bali pia ujumbe thabiti kwa vyama vingine na wananchi kuwa CCM bado inajiamini, na Dkt. Samia bado ana maono ya kulitumikia taifa.

Katika mazingira tulivu lakini yenye uzito wa kisiasa, msafara wake ulipokewa kwa nidhamu na hadhi, ukiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Alhaj Adamu Kimbisa.
Wakati huo huo, vyama vingine 17 vilivyopata fursa ya kuchukua fomu za urais pia vimeonesha dhamira ya kushiriki katika uchaguzi huu, akiwemo ACT-Wazalendo, CUF, NCCR-Mageuzi, UDP, ADC, TLP, na vingine vidogo kama NRA, UMD, na CHAUUMA.

Mchanganyiko huu unaonyesha uwiano wa vyama vya muda mrefu na vyama vipya, wote wakiwa na ndoto ya kuiongoza Tanzania.
Kampeni rasmi zinatarajiwa kuanza Agosti 28 , huku macho ya Watanzania yakisubiri kwa hamu majibu ya swali kuu: Je, Dkt. Samia ataandika historia kwa kupata muhula mwingine, au historia mpya itaandikwa?
