Na Kulwa Karedia, Jamhuri Media Musoma
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amesema ndani ya Mkoa wa Mara kuna watu wamenuna nuna, wanachochea na kusaidia wagombea wa vyama vya upinzani ili waikomoe CCM.
Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa mji wa Musoma mkoani Mara, wakati wa mkutano wake wa kampeni za uchaguzi mkuu leo Oktoba 9,2025.
Amesema kutokana na mwenendo huo, CCM hakomoki hata kidogo kwa sababu ipo kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi.

“Katika kuhakikisha na kuthibitisha hili,nawaomba ndugu zangu Oktoba 29 tunyanyuke kwa pamoja tuchague CCM, ukipeleka huko unakoshawishiwa umepeleka kura yako kwenye jimbo hiyo ziro na kama mtatoa huko kwenye jimbo litabaki kuwa na ziro, ukija huku mambo yako kwenye kitabu kidogo hiki cha mkoa wenu, kinasema kila wilaya itapata miradi gani au maendeleo gani,amesema.
Amesema atahakikisha anafufua Bandari ya Musoma ili ifanye kazi kwa sababu inategemewa kwa uchumi wa eneo.
Kuna bandari ya zamani sana ambayo imeachwa kutumika na nyingine inatumika, naomba niwaambie tumejipanga kuendeleza usafiri kwenye maji tutazifufua kwa sababu pale Mwanza tumejenga meli kubwa ya MV Mwanza ambayo itasafiri kutoka Mwanza kuja Musoma mpaka kwa majirani zetu Uganda.

Kwa msingi huo lzima tuzifufue zipokee meli kubwa kubwa na biashara iweze kushamiri ndani ya mikoa na nchi yetu kwa ujumla,amesema.
Amesema jambo jingine kubwa zaidi ni mradi ujio wa mradi wa ya kisasa ya SGR ambayo itajengwa kutoka Tanga-Arusha- Musoma yenye urefu wa kilomita 1,108.
Reli hii itakuja moja kwa moja Musoma inakuja na mapinduzi ya kiuchumi ndani ya mkoa wetu, kilichobaki baki hapa twendeni tukachaguwe CCM ili haya nayo yasema tuje tuyafanyie kazi,amesema.
Kuhusu hudma za kijamii, elimu, afya, barabara na mengine amesema wamejipanga vizuri kwenda kukamilisha miradi yote ambayo imeanza na itakayoanzishwa.

Nawahakikisha kama kuna suala la elimu mambo hajafika tunakwenda kukamilisha, afya hivyo hivyo,pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba,amesema.
Kuhusu suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi, Rais Samia amesema kupitia mradi wa TATIC serikali inajenga Tanzania nzima vituo vya mabasi na stendi za kisasa ili kutoa fursa ndogo ndogo kwa wafanyabiashara.
Kupitia mfuko wa halmashauri wa asilimia 10,umekuwa msaada mkubwa wa kujenga na kuwezesha wananchi kiuchumi, pamoja na hayo wakati nazindua kampeni tulisema tutaanzisha mfuko wa wafanyabaishara ndogo ndogo utaanza na shilingi bilioni 200, alafu tuone unavyokwenda, vijana wangu wa Musoma semeni mnataka kufanya biashara gani,amesema.

Amesema wamejipanga kurasimisha biashara ndogo ndogo ili zitambulike na kuwa rasmi ili wananchi wafaidike nayo.
Amesema kwa upande wa wafugaji serikali imetoa chanjo za wanyama kwa ruzuku hadi kuku wanachanjwa bure.
Kuhusu elimu, amesema serikali imeendelea kutoa elimu bila ada kutoka darasa la kwanza mpaka kidato cha sita ili kutoa unafuu kwa wazazi.
Eneo la tatu ni sekta ya uzalishaji, ,kunahitajika kuwapo na mipango ya kilimo cha umwagiliaji maji ambapo serikali itajenga skimu na mabwawa ili wananchi wewe kumwagilia.
Kwa upnde wa uvuvi, Rais Samia anasema wamechukua hatua ya kuwezesha wavuvi ili wazalishe zaidi. Anasema serikali imekuja na wazo la ufungaji wa samaki kwa njia ya mabwawa na vizimba.

Tumekuja na njia hizi mbili ambazo vijana wetu wanazifanya, tuzalishe samaki tuwaongeze samaki na tuweze kufanya biashara, yote haya baadae italeta maendeleo ya viwanda ndiyo maana tunataka kila wilaya iwe na kongani za viwanda ambazo zitaongeza thamani ya kile kinachofanyika kwenye eneo husika,amesema.
Kuhusu miundombinu, amesema ndani ya mkoa huo wameanza kujenga barabara mbalimbali zikiwamo zile ambazo ziko kwenye ilani na sizizokuwamo.
Katika hatua nyingine, amesema serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma ili ufikie viwanngo vya kutua ndege kubwa ambazo zitakwenda kibiashara.


