Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Uvinza
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema kama atachaguliwa tena atahakikisha atafungua fursa za uchumi kwa wakazi wa Uvinza.
Amesema fursa hizo ni pamoja na kujenga soko kwa ajili ya kina mama wajasiriamali ambao wengi wanafanya biashara ya kuuza maharage na mazao mengine.
Ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa kuomba kura,katika Kijiji cha Kazuramimba wilayani Uvinza mkoani Kigoma leo Septemba 13, 2025.
Amesema lengo la serikali ni kuboresha hali ya wanawake wajasiriamali kwa kujenga mabanda ya kisasa ya masoko, akishirikiana na Mbunge wa Viti Maalum, Zainabu Katimba.

“Kina mama ni wazalishaji wazuri, wanakosa masoko,tutawajengea mabanda bora ya kuuzia bidhaa zenu, kuboresha mazingira safi na salama,”amesema.
Amesema serikali imetumia zaidi ya Sh bilioni 13 kujenga shule mpya 34, hatua iliyowezesha upanuzi wa fursa za elimu na kuongeza udahili wa wanafunzi.
Amesema Sh bilioni 19 zimetolewa kwa ajili ya shule za sekondari, ambapo sasa idadi yake zimefika 31.
Amesema atajitahidi kuongeza upatikanaji wa mbolea ya ruzuku kwa ajili ya wakulima wa zao la maharage.
Amesema zao hilo limekuwa mkombozi mkubwa wa wakazi wa Wilaya ya Uvinza na mkoa huo.

Kwa upande wa nishati, Samia amesema vijiji vyote vya Uvinza vimeunganishwa na umeme, sasa kazi inayoendelea ni kufikia vitongoji.
Amese kaya zinazotumia umeme zimeongezeka kutoka 2,072 hadi 9,613.
“Haya ni mafanikio makubwa kufanikisha mpango wa umeme kwa wote,”amesema.
Kuhusu uvuvi amesema imetoa Sh milioni 442 kwa ajili ya mikopo kwa wavuvi wadogo. Amesema mradi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma umejengwa ili kufungua fursa za kibiashara na kukuza uchumi wa mikoa ya magharibi.

“Uvinza itakuwa na kituo kikubwa cha SGR. Ni fursa kubwa, tunaomba mjipange kuitumia kibiashara,” alisema.
Amesema serikali itakamilisha barabara za ndani kama ilani ya CCM inavyoelekeza, zikiwemo barabara za Nguluka na Uvinza, pamoja na ujenzi wa madaraja ya kupitisha mazao ya wakulima.







