Na Kulwa Karedia, JamhuriMedia, Bukombe
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amejipanga kuanzisha kiwanda cha kuchakata maziwa.
Ametoa kauli hiyo wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa wilaya ya Bukombe mkoani Geita wakati wa mikutano wa kampeni za uchaguzi mkuu leo Oktoba 12.

“Natambua Wilaya ya Bukombe ni wafugaji wazuri wa ng’ombe, sasa tunataka tuongeze ng’ombe wa maziwa, kwa msingi huo tutaanzisha kiwanda cha kuchakata maziwa ili yawe bidhaa na fedha ziingie mfukoni maisha yaendelee,”amesema.
Amesema serikali imedhamiria kuinua sekta ya maziwa.
Amesema mbali na kiwanda hicho, Serikali imejipanga kuongeza nguvu katika ujenzi wa majosho na machinjio ya kisasa.
“Tumeamua kuingia kwenye sekta ya maziwa tuiinue kwa sababu inagusa maisha ya wana Bukombe na Watanzania kiujumla,”amesema.
Kuhusu sekta ya Madini, Rais Samia amesema serikali imeboresha kwa kuweka mazingira yaliyosaidia wachimbaji kupata leseni.

Amesema kabla ya hapo wachimbaji wengi hasa vijana walikuwa wakiingia kwenye pori la Kigosi na kufanya shughuli za uchimbaji kwa njia panya na mwisho wa siku kuishiwa kukamatwa na vyombo vya dola.
“Ndugu zangu unapokuwa na mtoto mwenye tabia mbaya mama anapopika mboga anadokoa kipande cha nyama hupigwa,lakini kwenye zizi kuna ng’ombe au kondoo nitachukuwa mmoja nitachinja niwapikie nyama wale mpaka washibe .
“Viijana wangu wa Bukombe walikuwa wanakwenda kufanya shughuli ya uchimbaji kwa njia ya wizi ambayo haikuwa nzuri.
“Mungu alishusha madini haya ili yatusaidie, nikamtaka Doto Biteko akae na wenzake waone wanavyoweza kufanya ndiyo wakafikia hatua hii ambayo leo mnaiona,”amesema.
Amesema hali ndiyo inaakisi kauli mbiu ya chama hicho ya Kazi na Utu tunasonga mbele “Huku ndiyo kujenga utu wa Mtanzania kama kauli mbiu yetu inavyoelekeza, tumedhamiria kuwezesha vijana wengi wajiajiri kwenye eneo hili,”amesema.

Kuhusu kilimo, amesema wilaya hiyo ina wakulima wazuri wa mazao ya mahindi, mpunga na viazi ambao kwa muda mrefu walikuwa wanalilia msaada wa Serikali.
“Tulichokifanya ni kuleta ruzuku ya mbolea, pembejeo, tunataka tuchimbe mabwawa ya umwagiliaji maji ili wakulima wazalishe kwa wingi,”amesema.
Katika elimu,Rais Samia amesema anatambua vijana wa Bukombe wanahitaji chuo ambacho ujenzi wake unaendelea.
“Uwanja umejengwa mkubwa, mzuri na wa kisasa kwa nguvu ya Serikali na watu wengine waliojitolea, nawashukuru wote waliojitolea katika ujenzi huu, akiwamo Azam aliyetupatia taa,” amesema.

“Tufanye kazi tulinde uwanja huu na kulinda utu wa mwana Bukombe
“Nimekuja maalumu kuomba kura zenu, najua nisingekuja mngenipigia kwa mambo mazuri yaliyofanyika,lakini ungwana ni vizuri tuonane kama hivi,”amesema.
