Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema serikali yake ya awamu ya sita na awamu ya tano zimefanikiwa kutekeleza kwa vitendo Maono na Fikra za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kujenga Taifa imara linalojitegemea na kujali maendeleo ya watu.

Dkt. Samia ametoa kauli hiyo wakati huu ambapo leo Jumatano Oktoba 14, 2025 Tanzania inaadhimisha miaka 26 tangu kutokea kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Kiongozi na muasisi wa nchi aliyejenga misingi ya Taifa katika itikadi na falsafa za kuwaletea wananchi maendeleo na kujenga Taifa lenye uchumi jumuishi na lenye kujitegemea, akipigana vita dhidi ya Umaskini, maradhi pamoja na Ujinga.

“Tunapomzungumzia baba Taifa hatuwezi kumtenganisha na misingi ya kiitikadi na kifalsafa iliyojengwa na dhana mbalimbali. Alisisitiza kuwa maendeleo yote yenye maana hayana budi kuwalenga watu na ndiyo maana dira na mipango yetu yote ya maendeleo pamoja na ilani ya Chama Cha Mapinduzi inajielekeza kujenga Taifa linalojitegemea, lenye uchumi jumuishi na ustawi wa watu yaani maendeleo ya jamii, uwezeshaji wa kiuchumi na kukuza uchumi wa Taifa letu.” Amekaririwa akisema Dkt. Samia.

Oktoba 10, 2025 akiwa Butiama Mkoani Mara alipozaliwa na kuzikwa Baba wa Taifa Dkt. Samia alisema serikali yake imefanikiwa kutimiza maono na ndoto za Baba wa Taifa kwa vitendo kupitia miradi mikubwa ya Kimkakati ikiwemo ujenzi na ukamilishaji wa mradi wa Kimkakati wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, mradi unaozalisha Megawati zaidi ya 2000 za umeme na kuondoa kabisa changamoto za umeme.

Dkt. Samia ametaja miradi mingine kuwa ni Makao makuu ya nchi kuhamishiwa Dodoma kwa Mihimili yote ya nchi kuhamia Mkoani humo, ujenzi wa Mradi wa maji wa Same- Mwanga- Korogwe, ujenzi wa Bwawa la Mkomazi (Korogwe), ambalo kwasasa limefikia asilimia 50 pamoja na Bwawa la Kidunda ambalo kukamilika kwake litasaidia kutatua kero za Maji kwenye Mikoa ya Pwani, Dar Es Salaam, Pwani na sehemu ya Mkoa wa Morogoro.

“Baba wa Taifa aliliachia Taifa Misingi mizuri ya kifalsafa, kisera na kisiasa na kazi yetu sasa kama Viongozi ni kutafsiri misingi hiyo na fikra hizo katika mazingira ya sasa na Dira mipango na Ilani yetu ya uchaguzi inatafsiri fikra hizo kwa kujenga Taifa linalojitegemea, Jumuishi na lenye ustawi kwa wananchi wote na kukuza sekta za kiuchumi. Kwa ufupi zile ndoto za Mwalimu Nyerere tunaendelea kuzitekeleza kwa Vitendo.” Amesema Dkt. Samia.

Kwa upande wao wananchi wa Wilaya ya Butiama wamemshukuru Dkt. Samia kwa kutimiza ndoto za Mwalimu Nyerere za kudumisha amani na utulivu nchini pamoja na kujenga chuo cha Kilimo Wilayani Butiama, chuo ambacho hakikujengwa kwa miaka mingi iliyopita na leo Dkt. Samia tayari amesimamia ujenzi wa chuo hicho kitakachogharimu Bilioni 102.5, wakisema Chuo hicho kitatoa fursa ya masomo kwa Vijana na kukuza sekta ya Kilimo kwa Wilaya ya Butiama na Tanzania kwa ujumla.