Na Kulwa Karedia-Dar es Salaam
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amewaasa vijana wa Tanzania kutokubali kudanganywa na kuwataka washushe munkari.
Rais Samia ametoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu katika majimbo ya Mbagala, Kigamboni, Temeke na Chamazi kwenye viwanja wa Buza Tanesco wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam leo Oktoba 23,2025.
Nawasihi vijana wa kitanzania msidanganywe, ukichukua Afrika Mashariki, kati na kusini, Tanzania ni mahala tulivu upo kwenye nchi yenye jina, sifa zake yenye kuendeleza watu wake.
Msidanganywe wale walioko nje huko wasiwandanganye hapa mko pazuri kweliweli, mkipata fursa ya kuingia kwa majirani zetu mkaangalie vijana wenzenu wanavyokula ngumu unaweza kusema narudi Tanzania ndiyo kwetu. Niwaambie vijana sisi wazazi wenu tunapita nchi hii inawategemea ninyi tunatarajia tuwaachie nchi hii muiendeshe kama tunavyoiendesha sisi.
Kwa msingi huo vijana wa Tanzania msidanganywe hata kidogo na katika kuendesha nchi tumetengeneza mifumo mizuri sana ambayo kila baada ya miaka mitano tunachaguana nani atuendeshe katika nafasi ipi, hakuna maeneo mengine wanangu, nawaomba vijana wa Kitanzania tulizeni munkari,amesema.
Amewataka kukaa vizuri kwa sababu Tanzania ni mali yao na kuwa si mali ya mtu mwingine wala mwenye cheti anayeweza kusema ni mali yake.
Wengine wanasema sisi tuna wakilisha wananchi, hivi wananchi ni kina nani ni ninyi hapa na wengine hakuna mwenye miliki ya wananchi, tunapeana majukumu wewe shika hili na mwingine anashika lile, nawaomba sana msiaharibu nchi yenu, amani ya nchi yenu fuateni serikali yenu inavyowaelekeza, fuateni Katiba inavyowaelekeza, fuateni sheria za nchi zinavyotaka, mtaishi salama na kwa amani wala hatamsumbuliwa,amesema.
Kutokana na hali hiyo, awamesihi vijana kujitokeza kwenda kupiga kura kwa sababu mama na vyombo vya ulinzi na usalama viko macho.
Kama yamewashinda ni wao, sisi tunaendelea na ujenzi wa nchi yetu, kuweni na amani kabisa,amesema.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema wilaya za Temeke na Kigamboni zimekuwa na ukuaji wa kasi wa wananchi unaokwenda sambamba na uhitaji wa huduma mbalimbali.
Wilaya hizi ni mwenyeji wa miradi mikubwa ya viwanda na Bandari ya Dar es Salaam, maonyesho ya kimataifa ya Dar es Salaam na mambo mengi bila kusahau uwanja wa michezo wa Mkapa. Haya ni maeneo muhimu kwa uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.
“Mwasisi wa Taifa letu Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alituambia ili nchi ipate maendeleo lazima kuzingatia mambo manne, watu, ardhi, siasa safi na uongozi ulio bora ndani ya nchi. Kwa muda mwingine tumekuwa tukiyafanyia kazi kwa kasi ndogo.
Tumeamua CCM na ndivyo inavyotuelekeza kwenye Ilani iliyopita, tunayokwenda kuitekeleza miaka mitano ijayo, tujikite sana kwenye watu, tuendeleza watu, utu wa mtu, tuujenge utu wa Mtanzania, tuheshimishe utu wa Mtanzania ili asimame kuwa mtu ana mahitaji yake ya lazima ambayo kama chakula, huduma za afya, maji safi, elimu, umeme umwakie na makazi.
Mambo haya yote tumeyafanyika kazi vizuri sana, kwenye makazi ninyi ni mashahidi watu wanajenga, mashirika yetu ya serikali yanajenga. Kwa mfano pale Mtoni kuna nyumba 400 Shirika la Nyumba la Taifa linajenga na kazi inaendelea Tanzania nzima. Kwa mahitaji muhimu ya wanadamu serikali yenu imefanya vizuri sana.amesema.
Kuhusu eneo la uchumi, Rais Samia amesema serikali imefanya kazi nzuri kwa kujenga uchumi mkubwa na mdogo kwa watu wa kipato cha chini kwa kutoa mikopo na mitaji.
Katika hili tumejitahidi mno tumejenga stendi za mabasi, masoko, maeneo maalumu ya wafanyabiashara wadogo wadogo, halmshauri zetu tumewaka asilimia 10 kwa ajili ya vijana na watu wenye ulemavu tumefanya kazi nzuri sana,amesema.


