Na Kulwa Karedia Jamhuri Media, Pemba
MGOMBEA urais Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi kutokubali kuchokozwa.
Amesema wakichokozeka watahatarisha amani ya nchi kwa sababu ya uchaguzi jambo ambalo halina tija Dk. Samia ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupigakura Oktoba 29 mwaka huu kama wanavyojitokeza kwenye mikutano yake.
Amerudia kauli yake kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kulinda amani ya nchi
Amesema kipindi hiki cha uchaguzi wapo baadhi ya watu wanatamani kuvuruga amani na kuwasisitiza kutokubali kuchokozeka.

Akihutubia maelfu ya wananchi waliojazana uwanja wa Gombani ya Kale, Mkoa wa Kusini Pemba Septemba 20,2025, Rais Samia amesema siku ya kupiga kura hakutakuwa na vurugu.
Amesema.badala yake wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi kutimiza takwa la kidemokrasia kuchagua viongozi wanaowataka kama ilivyo kawaida
“Msichokozeke, kuweni kama mimi mama yenu, dada yenu na bibi yenu ninachokozeka sana lakini sikubali kuchokozeka.
Tusiende kuvunja amani ya nchi, tutunze amani na utulivu. Tunapochokozwa tusichokozeke,’ amesisitiza
Ameongeza “Tarehe 29 Oktoba hakutakuwa na vurugu, vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vyema kulinda nchi na ninayezungumza hapa ni Amiri Jeshi Mkuu.”
Amesema serikali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imejitahidi kusimamia utulivu wa kisiasa na amani ambapo hakuna vurugu zozote zilizosikika.
“Wenzetu wanayolalamikia hakuna lisilozungumzika.Tutakaa tutazungumza, tusiende kuleta vurugu kuvunja amani kwa sababu hili halikufanyika. Tukapige kura, turudi nyumbani tusubiri matokeo,”amesema.
Amesisitiza kuwa serikali za CCM ni serikali za vitendo na siyo maneno kama watu wanavyofikiria.
Amesema Pemba kila kukicha imekuwa ikibadilika ikiwa ni matokeo ya miradi ya maendeleo inayopelekwa kisiwani humo.
“Serikali za CCM vinafanyakazi kwa vitendo na siyo blah..blah…kila nikija Pemba mambo yanaendelea kubadilika,”amesema.

Amesema baadhi ya miradi mikubwa inayotekelezwa ni ujenzi wa uwanja wa Ndege Pemba ambao utakuwa wenye hadhi ya kimataifa.
Amesema uwanja huo, baada ya kukamilika ndege kubwa za abiria na mizigo zitatua, hivyo kufungua zaidi uchumi wa Pemba.
Amesema watalii na ndege za mizigo watafika moja kwa moja Pemba badala ya kutua unguja.

Alitaja miradi mingine ni ujenzi wa barabara ya Chake chake – Mkoani ambao fedha zake zimeshapatikana.
Amesema ujenzi wa Bandari ya Shumba utarahisisha shughuli za uchukuzi baina ya Pemba na Mombasa hatua ambayo itaondoa changamoto ya usafiri.
Amesema wakazi wa maeneo hayo watatumia boti za kisasa badala ya usafiri wa vidau ambavyo usalama wake ni mdogo.

Amesema kisiwa hicho, kimenufaika kupitia ujenzi wa shule za ghorofa ikiwemo eneo la Kojani.
“Ndiyo maana tunapata ujasiri kwa kujiamini kuomba ridhaa ya kuchaguliwa tena.
Tunaamini tumeweza kufanya makubwa, makubwa mengine zaidi tunaweza kuyafanya. Tupeni mitano mingine tufanye makubwa zaidi.
“Tunafanyakazi kustawisha maisha ya wananchi. Mtu akifanyakazi ipasavyo atapata ujira kisha kufanya maendeleo. Kazi na Utu maana yake ni kusonga mbele,” alisisitiza.

Amesema Serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar zinafanyakazi pamoja kukabiliana na changamoto mbalimbali za kidunia.
Alitaja baadhi ya miradi ni ule wa kulinda maeneo ya ardhi yasiharibiwe na bahari hali inayochangiwa na uharibifu wa mazingira duniani.
Amesema serikali imekuwa ikisisitiza matumizi ya nishati safi ikiwa ni mkakati ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi kupikia.






