Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
BODI ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) imetakiwa kuweka mikakati ya kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili mfuko uchangie katika kutoa huduma bora zaidi ikiwemo kuongeza uzalishaji ajira kwa sekta binafsi.
Akizungumza katika kikao hicho, juzi Jijini Dodoma Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu alisema Serikali kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuanzisha na kuimarisha mfumo jumuishi wa hifadhi ya jamii utakaojumuisha sekta isiyo rasmi.
“Hatua hiyo itachochea uwekezaji katika miradi ya maendeleo, kuongeza wigo wa ulinzi wa kijamii na kuimarisha uzalishaji wa ajira kwa Watanzania wengi” amesema.
Sangu alisema Serikali kuanzia mwezi Julai mwaka huu itaanza utekelezaji wa Dira 2050 ambapo kwa sekta ya hifadhi ya jamii dhima mojawapo ni kuhakikisha ukuaji wa Uchumi Jumuishi na uzalishaji wa ajira unapewa kipaumbele kupitia sekta binafsi.
Katika hatua nyingine alisema katika mpango wa kwanza wa maendeleo wa miaka mitano utakaochangiwa sekta binasfsi inatakiwa kuchangia asilimia 70 ambapo Mfuko wa WCF unatakiwa kuongeza wigo wa kuandika wanachama toka sekta binafsi ili kiwango cha uchanguaji kikue zaidi.
“ Tuitazame sekta binafsi kama kiungo cha kukuza Uchumi ambapo mfuko wa WCF unapaswa kubuni na kuwekeza kwenye miradi ya kimakakati ambayo itaongeza kasi ya uzalishaji ajira ili mfuko upate wachangiaji wengi zaidi na kuufanya uendelee kuwa himilivu” alisisitiza Waziri Sangu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Renata Rugarabamu alimweleza Waziri kuwa mfuko huo ni himilivu na kwamba unaendelea kutoa huduma zake kwa wafanyakazi kwa weledi na ubora.
Rugarabamu aliongeza kusema Mfuko wa WCF utaendelea kuhakikisha wafanyakazi waliopata majanga inawapa fidia ili waweze kurudi katika jamii kuendelea kutoa mchango wao kwenye ukuaji wa uchumi ambapo alibainisha kuwa mfuko umeongezeka toka shilingi Bilioni 26 mwaka 2024 hadi shilingi Bilioni 51 mwaka 2025 hatua inayoufanya uwe himilivu.
Waziri Sangu alikutana na Bodi hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kuwa Waziri mwenye dhamana ya sekta ya kinga ya jamii ambapo Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni moja wapo. Taasisi zingine zinazotekeleza kinga ya jamii ni Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).


