Na Aziza Nangwa,JamhuriMedia, Dar es Salaam

Chama cha Sauti ya Umma (SAU) kimesema kwenye ilani yake ya mwaka 2025-2030 kwamba kitaushirikisha umma kulinda vyanzo vya maji pamoja na kutekeleza miradi yote ya maji na kujenga mabwawa makubwa kwa ajili ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua yatakayotumika kwa binadamu, mifugo na kilimo cha umwagiliaj.

Pia kimesema serikali yake itahakikisha wananchi wanapata huduma ya maji na safi na salama bure na changamoto ya upatikanaji wa maji nchini itaondolewa kupitia uanzishwaji wa miradi mbalimbali ya maji katika maeneo ya mijini na vijijini.

SAU kimesema hadi sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya kaya takriban milioni 15, huku tafiti zikionesha kwa wastani mtu mmoja hutumia maji safi kati ya lita 15 hadi 25 kwa siku.

Kimeeleza kuwa takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 50 ya maji hupotea kabla ya kuwafikia watumiaji, sawa na zaidi ya lita milioni 200 zenye thamani inayozidi Sh bilioni 350 kila mwaka.

“Kwa kuwa tatizo la maji litakuwa limepati wa ufumbuzi, mama na dada zetu waliokuwa wakikesha kwenye foleni za maji watapata muda wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi wa familia na taifa kwa ujumla,” amesema.