Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mkurugenzi wa Shirika la Foundation for Disabilities and Hope (FDH), Michael Salali, amesema uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ni ushahidi thabiti kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kwa dhati kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika ajenda kuu za maendeleo.

Ametoa kauli hiyo jijini Dodoma, mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuzindua rasmi dira hiyo katika hafla ya kitaifa iliyofanyika Julai 17, 2025.

Salali amesema mchakato wa maandalizi ya Dira hiyo ulijikita katika ushirikishaji wa makundi yote ya jamii, ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu ambao mara nyingi wamekuwa wakiachwa nyuma katika kupanga mustakabali wa taifa.

Amesema kuwa kwa mara ya kwanza, mawazo na changamoto za watu wenye ulemavu zimezingatiwa rasmi ndani ya dira ya maendeleo ya taifa.

“FDH na watu wenye ulemavu kwa ujumla tunaamini hii siyo tu dira ya kitaifa bali ni tumaini jipya kwa wenye mahitaji maalum kwa kuwa inaonesha kuwa hatujaachwa nyuma Sauti zetu sasa zinasikika na zinatekelezeka,” amesema Salali.

Ametaja baadhi ya changamoto za wenye ulemavu kuwa zinaenda kutatuliwa moja kwa moja ndani ya dira hiyo .

“Tunaamni Dira hii itajibu ajira, elimu jumuishi, huduma za afya rafiki kwa watu wenye ulemavu, miundombinu isiyo rafiki, pamoja na kutengwa kwenye fursa za mikopo na teknolojia kwa kuwa dira hii inaweka msingi wa kushughulikia changamoto zote kupitia sera shirikishi na uwekezaji katika rasilimali watu, “ameeleza.

Mbali na hayo amesisitiza kuwa watu wenye ulemavu tayari wana Dira mahsusi inayoelekeza namna ya kutatua matatizo yao, na kwamba Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 inapaswa kuendana na nyaraka hiyo ili kuhakikisha hakuna kundi linalosahaulika.

“Tunatoa rai kwa Watanzania wote wenye ulemavu kuisoma na kuielewa dira hii,tukifahamu yaliyomo, tutajua tunapaswa kudai nini na kwa namna gani,” ameeleza.

Aidha amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ya Awamu ya Sita kuwa imefanya hatua za wazi katika kuinua kundi la watu wenye ulemavu.

Ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya elimu jumuishi,Kutoa ajira serikalini kwa watu wenye ulemavu,kusambaza vifaa saidizi mashuleni na hospitalini,Kuboresha sheria na sera kuhusu usawa, na Kuwezesha ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye mabaraza na kamati za kitaifa.

Mkurugenzi huyo wa FDH amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha utekelezaji wa dira hiyo unaenda sambamba na matakwa halisi ya watu wenye ulemavu, ikiwemo kufanya tafiti, kutoa elimu kwa jamii, na kuibua vikwazo vinavyohitaji kufanyiwa kazi.

Salali ametoa rai kwa mashirika mengine ya kiraia kufanya kazi kwa karibu na Serikali ili kuhakikisha mabadiliko yanakuwa ya kweli na yanayogusa maisha ya watu moja kwa moja.

“Tanzania haiwezi kufikia maendeleo ya kweli bila kujumuisha kila kundi,Dira hii ni fursa ya kulinda utu na haki zetu kama binadamu,” amesisitiza.

Uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya 2050 umehudhuriwa na viongozi wa Serikali, dini, sekta binafsi, mabalozi na wawakilishi wa makundi maalum, wakiwemo watu wenye ulemavu.

Aidha Dira hiyo inatajwa kuongozwa na misingi mitano mikuu ambayo ni Demokrasia, haki na uhuru; utu na mshikamano; matumizi bora ya rasilimali; utamaduni na maadili ya taifa; pamoja na ushiriki wa wananchi katika maendeleo.