Na Mwandishi Wetu
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Vienna katika nyanja za sayansi na teknolojia, ikiwemo nishati ya jua, ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Hayo yameelezwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma) kutoka UDSM, Prof. Rose Upor alipofanya mazungumzo na Ujumbe wa Austria ulioongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya kisiasa, Mhe. Balozi Dkt. Hannah Liko, ulipotembelea chuoni hapo Machi 24, 2026 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika sekta ya elimu kati ya Tanzania na Austria.
Prof. Upor amesema ili kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo kati ya UDSM na Chuo Kikuu cha Vienna, kuna umuhimu wa kuongeza ufadhili wa masomo katika kada mbalimbali pamoja na kubadilishana wataalamu watakaoweza kufundisha hata kwa njia ya mtandao.
Naye Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Vienna, Balozi Naimi S.H. Aziz, amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Austria katika sekta ya elimu una mchango mkubwa katika kukuza ujuzi, kuimarisha taasisi na kuongeza ubora wa huduma nchini.
Kwa upande wake, Dkt. Liko amepongeza ushirikiano uliopo kati ya UDSM na Chuo Kikuu cha Vienna, huku akipendekeza kuanzishwa kwa mafunzo ya lugha ya Kijerumani katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Amesema kuwa kuimarika kwa ushirikiano katika sekta ya elimu kutachangia maendeleo ya kiuchumi na kidiplomasia kwa mataifa yote mawili.
Ushirikiano kati ya UDSM na Chuo Kikuu cha Vienna unalenga maeneo manne makuu ya kimkakati, yakiwemo ubadilishanaji wa wanafunzi ili kuwapatia uzoefu wa kimataifa, ubadilishanaji wa wafanyakazi wa kitaaluma na kiutawala, utekelezaji wa tafiti za pamoja zinazogusa changamoto za kimataifa kama utawala bora na maendeleo endelevu, pamoja na uchapishaji wa kazi za pamoja za kitaaluma ili kuhakikisha mitazamo ya Afrika inawakilishwa vyema kimataifa.











