Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Shule ya Sekondari Pangani , Manispaa ya Kibaha imefanya zoezi la kupanda miti zaidi ya 344 ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhimiza taasisi za elimu kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Zoezi hilo limehusisha wanafunzi, walimu, wadau wa mazingira pamoja na viongozi wa Serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Pangani, kwa lengo la kuifanya shule hiyo kuwa ya kijani yenye mazingira bora na ya kuvutia.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Pangani, Tatu Mwambala, alieleza miti hiyo ni ya kivuli na mbao, ambapo miti 220 imetolewa na kitalu cha Manispaa ya Kibaha, miti 110 imetolewa na Wakala wa Misitu kupitia Shule ya Sekondari Msangani II, huku miti 14 ya matunda ikinunuliwa na shule.

Alisema miti hiyo itasaidia kukuza stadi za uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi, kutoa kivuli na kuchangia afya bora kupitia ulaji wa matunda kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kadhalika Mwambala alieleza kuwa shule hiyo ina Klabu ya Mazingira yenye wanafunzi 48, wakiwemo wasichana 26 na wavulana 22, ambao kwa kushirikiana na wanafunzi wengine wanahakikisha mazingira ya shule yanakuwa safi muda wote.
Diwani wa Kata ya Pangani, John Katele, alisema zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Pangani ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na mikakati ya mkoa na manispaa katika kuhifadhi mazingira na kufanikisha mpango wa kupanda miti milioni 1.5.
“Kupitia zoezi hili tunatekeleza maelekezo ya Serikali na Ilani ya chama kwa kuhakikisha mazingira yanatunzwa,” alisema Katele.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Pangani, Benjamin Mputu, alisema mazingira ni uhai hivyo jamii inapaswa kuyatunza kwa lengo la kuongeza uoto wa asili na kuboresha ustawi wa mazingira.

Naye Ofisa Kilimo wa kata hiyo, Omary Ngulengule, alibainisha zoezi hilo limewapa wanafunzi na walimu elimu ya vitendo kuhusu uchimbaji wa mashimo, matumizi ya mbolea pamoja na upandaji sahihi wa miti.
Alisema lengo ni kuwafanya wanafunzi kuwa mabalozi wa utunzaji wa mazingira kuanzia shuleni hadi katika jamii wanazotoka.
Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Pangani, Stanley Amos, alishukuru kwa elimu waliyoipata kupitia zoezi hilo na kusema watakuwa mabalozi kwa familia na jamii katika kuhamasisha upandaji miti na utunzaji wa mazingira.







