Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Kupinga Dawa za Kulevya Duniani, akisisitiza kuwa tatizo hilo ni tishio la moja kwa moja kwa maendeleo ya taifa, hususan kwa vijana.

Akizungumza na waandishi wa habari leo June 24,2015 jijini Dodoma, Senyamule ameeleza kuwa maadhimisho hayo yatafanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Juni 24 hadi 26, 2025, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Jakaya Kikwete (JNICC).

Aidha amesema maadhimisho hayo , yatahitimishwa na mgeni rasmi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Maadhimisho haya ni ya kipekee na ni fursa adhimu kwa jamii kujifunza, kupata elimu sahihi juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya, na kuona juhudi kubwa zinazofanywa na serikali pamoja na wadau katika kuzuia janga hili,” amesema

Amefafanua kuwa maonesho ya kitaasisi mbalimbali pamoja na kongamano la vijana vitakuwa sehemu ya maadhimisho hayo.

“Kupitia kongamano hilo, vijana watajadili changamoto, fursa, na mbinu mbadala za kushiriki kikamilifu katika mapambano haya,tunahitaji kuwasikiliza vijana wetu, kuwapa dira, na kuwawezesha kuwa chachu ya mabadiliko,” ameongeza.

Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa karibu kati ya serikali, sekta binafsi, na jamii kwa ujumla.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwa ya aina yake, yakikusanya nguvu ya taifa katika kukabiliana na tatizo linaloathiri si tu afya za watu, bali pia ustawi wa uchumi na maendeleo endelevu ya nchi.