Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Singida
Serikali ipo mbioni kuandaa Sera ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria itakayoweka misingi ya kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi kote nchini.
Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, wakati wa uzinduzi wa kliniki ya huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa bure na Serikali, uliofanyika mkoani Singida.

Kliniki hiyo ni muendelezo wa kliniki ya awamu ya kwanza iliyozinduliwa hivi karibuni mkoani Morogoro .
Dkt. Homera amesema kuwa kliniki hizo ambazo zitaendelea katika mikoa mingine zinalenga kutatua migogoro mbalimbali ikiwemo ya ndoa, ardhi, mirathi na ukatili wa kijinsia kupitia taasisi za Serikali zikiwemo Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Amesema Sera hiyo itajikita katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utatuzi wa migogoro, kuanzisha na kuendesha Madawati ya Msaada wa Kisheria katika ngazi za halmashauri, kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali kupitia makubaliano.
Lakini pia kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kuhakikisha Daftari la Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria linahuishwa, kuwatumia kikamilifu Mawakili wa Serikali katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria.

Xx
“Sera hii itaweka msingi imara wa kuhakikisha wananchi wanapata msaada wa kisheria kwa ufanisi na kwa wakati,” amesema Dkt. Homera.
Ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma za msaada wa kisheria, huku mpango ukiwa ni kuzifikia halmashauri zote katika mikoa yote nchini.
“Chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, tutafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tunazifikia mikoa yote nchini,” amesema.
Ameongeza kuwa baada ya Morogoro na Singida, ratiba itaendelea katika mikoa mingine, na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi pindi huduma hizo zitakapowafikia katika maeneo yao.
Aidha, Waziri Homera ameipongeza RITA kwa utekelezaji wa mpango wa utoaji wa vyeti vya kuzaliwa ndani ya saa 48 za kazi kwa kutumia mfumo wa kidijitali wa e-RITA.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Bi. Zainab Katimba, amesema wizara hiyo imeanzisha kituo cha huduma kwa mteja kinachopatikana kupitia namba 0262160360, ambacho kimekuwa kikisaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu namna ya kuripoti na kushughulikia matukio ya ukatili wa kijinsia.
Amesema msaada wa kisheria ni nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kuwa unaimarisha mifumo ya utoaji haki na kujenga jamii salama yenye usawa wa kijinsia.
“Hivyo, nitoe rai kwa wananchi wote kuungana kwa pamoja kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia unaowaathiri zaidi wanawake na watoto,” amesisitiza Bi. Katimba.
Naye Meneja wa Usajili wa Vizazi, Vifo, Ndoa na Talaka kutoka RITA, Bi. Patricia Mpuya, amesema kuwa katika kliniki hizo wanatoa huduma za usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa, elimu ya ndoa na talaka pamoja na uandishi na uhifadhi wa wosia.
Amesema RITA imepokea jumla ya maombi 122,000 ya vyeti vya kuzaliwa kuanzia Desemba 15 mwaka jana, ambapo maombi 110,000 sawa na asilimia 91 tayari yameshafanyiwa kazi na wananchi kupokea vyeti vyao ndani ya saa 48 za kazi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, mmoja wa wananchi, Bw. Mohamed Amasi, amesema kliniki hiyo imemsaidia kupata elimu ya kutambua haki zake za msingi na namna ya kuzitetea kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Bi. Salma Ramadhani, mkazi wa kijiji cha Mangida, Halmashauri ya Wilaya ya Singida, ameipongeza Serikali kwa kuanzisha kliniki hiyo na kuomba huduma hizo zisishie mijini pekee bali ziwafikie wananchi wa vijijini ili kuongeza uelewa wa haki za kisheria kwa wananchi wengi zaidi.

