Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbarali
Wakazi wa Kata ya Ihahi, Wilaya ya Mbarali, wameishukuru Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), kwa hatua ya kujenga miundombinu ya Umwagiliaji ikiwemo mifereji kupitisha maji pamoja na kuziba makorongo yaliyokuwa yakisababisha madhara makubwa kwa wananchi.
Akizungumza na wananchi wa kata hiyo, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Ndugu Magdalena Sikwese, ambaye ni Afisa Tarafa ya Ilongo, amesema Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeanza kutekeleza mradi huo ili kukabiliana na changamoto sugu ya makorongo makubwa yaliyokuwa yakikatiza maeneo ya wananchi na kusababisha maji kupita kwa kasi kipindi cha mvua na kuleta mafuriko.

Amesema adha hiyo imewatesa wananchi wa Ihahi kwa miaka mitano mfululizo.
“Hali hii ilikuwa ikiharibu miundombinu, mashamba na makazi ya watu kwa zaidi ya miaka mitano na kusababisha mateso kwa wananchi,” amesema.
Pia amesisitiza hatua hiyo ni sehemu ya jitihada endelevu za Serikali kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi bila kukumbwa na madhara yanayosababishwa na mafuriko.
Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Ihahi wameeleza kuwa kabla ya mradi huo walikuwa wakikumbana na changamoto kubwa hasa wakati wa mvua kali, ambapo maji yalikuwa yakibeba mifugo, kuharibu mazao na kuathiri biashara ndogondogo.

Wameongeza kuwa zaidi ya wananchi 119 wamekuwani wahanga wa changamoto hiyo, jambo lililowafanya washindwe kuendelea na shughuli zao kama kawaida hali iliyokuwa ikiwaathiri kiuchumi.
Aidha Wananchi hao wamesema kuwa ujenzi wa mifereji uliofanywa na NIRC na kuziba makorongo umerejesha matumaini, kwani sasa wanaweza kufanya shughuli zao bila hofu ya mafuriko.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Mbeya, Abdallah Banzi, ametoa wito kwa wakazi wa Mbalali kuepuka kufanya shughuli za kilimo katika maeneo jirani na vyanzo vya maji na kuacha kuchimba au kuziba njia za kupitisha maji bila utaratibu.
Amesema vitendo hivyo vimekuwa vikiharibu mfumo wa maji na kuchangia kuongezeka kwa makorongo.

Hata hivyo, Tume imetumia zaidi ya shilingi Milioni 731 katika ujenzi huo, ulioanza Oktoba mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Januari 2026, lengo ni kuhahakikisha inasaidia wananchi kuondokana na adha ya mafuriko iliyokuwa ikiwakabili.






