▪️Waziri Mavunde aelekeza kuanza mchakato wa mabadiliko ya sheria

+Aelekeza kanuni kubadilishwa ili kupunguza tozo kwa hekta kufikia 20,000.

▪️Wazalishaji Chumvi wampongeza Rais Dk. Samia kwa ujenzi wa kiwanda cha mkoani Lindi

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali ipo mbioni kutambulisha leseni mpya ya uzalishaji wa chumvi na kuiondoa katika kundi la madini.

Hatua hiyo inalenga kuchochea ukuaji wa tasnia ya uzalishaji chumvi nchini.

Hayo yamesemwa leo jijini hapa wakati Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alipofanya kikao na uongozi wa Chama cha Wazalisha Chumvi Tanzania (TASPA).

“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametupa maelekezo mahsusi kuwawezesha wachimbaji wa madini na wazalishaji wa madini chumvi ili kuchochea ukuaji wa sekta ya madini.

“Serikali imesikia kilio chenu cha muda mrefu cha uwepo wa leseni moja ya uzalishaji wa Chumvi ambayo itasaidia kumwendeleza mzalishaji chumvi kwa kupunguza gharama za uzalishaji na kuyaondoa madini chumvi katika kundi la madini mengine.

‘Naelekeza kuanza mara moja mchakato wa mabadiliko ya sheria ili kuruhusu uanzishwaji wa leseni maalumu ya uzalishaji chumvi ambayo pia tozo yake kwa hekta iangaliwe upya kufikia Sh 20,000 kutoka kiwango kilichopo sasa.

“Dhamira ya serikali ni kuona wazalishaji wa chumvi wanaongeza tija na kufikia hatua ya kumiliki viwanda vya uchakataji na usafishaji chumvi nchini ili chumvi yetu iwe yenye ubora na shindani,” amesema Mavunde.

Aidha Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Eng. Yahaya Samamba ameipongeza TASPA kwa kazi ya kuwaendeleza na kuwasimamia wazalishaji chumvi na kuahidi ushirikiano wa kutosha kutoka Wizarani katika utatuzi wa changamoto za wanachama wake.

Akitoa maelezo yake,Mwenyekiti wa TASPA Bi. Hawa Ghasia ameipongeza wizara ya madini kwa utaratibu wa kuwasikiliza wadau na kutafuta suluhisho ya changamoto zao na kutumia fursa hiyo kumpongeza kipekee Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kusikia kilio cha wazalishaji wa chumvi kwa kujenga kiwanda cha Kuchakata na kusafisha chumvi kinachojengwa mkoani Lindi na Shirika la Madini la Taifa(STAMICO).