Na Mwandishi wetu– WAF, Dar es Salaam.
Wizara ya Afya imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kufuatilia ushauri wa kitaalam ili kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali kama ilivyoelezwa katika taarifa kwa umma ya Mganga Mkuu wa Serikali hivi karibuni
Hayo yamebainishwa leo Februari 27, 2026 Jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa alipofanya ziara ya kimakakati katika hospitali ya Rufaa Mkoa Amana kwa lengo la kukagua utolewaji wa huduma za afya pamoja na maendeleo ya uboreshaji wa miundombinu ya hospitali hiyo
Aidha amesema, Serikali bado inaendelea kufuatilia kwa ukaribu juu ya mienendo ya magonjwa mbalimbali kama kipindupindu, Dengue na UVIKO-19 hususani katika kipindi hiki cha mvua huku akisistiza kwamba hakuna kisa chochote UVIKO, cha mgonjwa aliyelazwa katika hospitali nchini

“Napenda kuwahakikishia wananchi na Watanzania wote Serikali yenu ipo makini na inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa maambukizi ya UVIKO-19 nchini na kimataifa, lakini pia tunasisitiza umuhimu wa kila mmoja kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia ushauri wa kitaalamu unaotolewa na wataalamu wa afya ili kulinda afya binafsi na ya jamii kwa ujumla,” amesema Mhe. Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa amewataka Watanzania kujiandikisha na kulipia bima ya afya kwa wote sababu gharama za matibabu zinaweza kuwa kikwazo kwa wananchi wa hali ya chini hasa wanapohitaji kufanyiwa huduma za kibingwa na kibingwa bobezi
Waziri Mchengerwa amesema kuwepo kwa bima ya afya kwa wote kuendana sanjari na upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya na hospitali ili kukamilisha dhamira ya serikali katika kurahisisha huduma za afya kwa wananchi
Katika ziara hiyo, Mhe. Mchengerwa ameambatana na Katibu Mkuu Dkt. Seif Shekalaghe pamoja na menejimenti ya Wizara ya Afya, ambapo alikagua hali ya upatikanaji wa huduma, kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi na wagonjwa, na kueleza mikakati madhubuti ya serikali katika kuimarisha ubora na ufanisi wa huduma za afya kwa wananchi.





