Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imetoa wito kwa wawekezaji wa kimataifa kuwekeza nchini kwa kiwango kikubwa na katika miradi ya kimkakati, ikisisitiza kuwa haivutii wawekezaji wanaokuja kushindana na Watanzania kwenye biashara ndogondogo.
Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini.
Profesa Mkumbo amesema kuwa serikali haitarajii kuona mwekezaji wa nje akija kuanzisha duka la viatu au kuuza nyanya, bali anatarajiwa kuleta mitaji mikubwa na miradi yenye tija kwa uchumi wa taifa pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania.
Amesema hatua inayofuata ni kukutana na wadau wa biashara na uwekezaji katika mikoa 16 ya Tanzania, iliyogawanywa kwa kanda, ili kukusanya maoni juu ya maeneo yanayohitaji kuboreshwa kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuvutia wawekezaji zaidi.
Mikoa itakayohusishwa katika zoezi hilo ni pamoja na Arusha, Dodoma, Mwanza, Kigoma, Mtwara na Dar es Salaam. Maeneo haya yatatumika kama vituo vya kukusanya maoni kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wawekezaji wa ndani na nje, pamoja na wananchi wa kawaida.
“Lengo letu ni kuhakikisha tunakusanya maoni kutoka kwa wadau wote ili mkakati unaoandaliwa uakisi matarajio na mahitaji yao, na kuvutia zaidi wawekezaji wa kimkakati,” amesema Prof. Mkumbo.
Aidha, ameyataka mashirika na vyama vya wafanyabiashara na wawekezaji kote nchini kushiriki kikamilifu kwa kutoa maoni yao kuhusu namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu ya Kuandaa Mkakati huo, Profesa Faustine Kamuzora, amesema kwa kipindi cha miaka sita iliyopita serikali imekuwa ikitekeleza awamu ya kwanza ya mpango wa maboresho ya mazingira ya biashara na uwekezaji, unaotarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
Prof. Kamuzora amesema tathmini ya utekelezaji wa mpango huo imebaini mafanikio pamoja na changamoto kadhaa ambazo serikali imelenga kuzifanyia kazi katika awamu ijayo, ikijikita zaidi kwenye maeneo yaliyoonesha mafanikio.
Mpango huu unalenga kuimarisha uchumi wa taifa kupitia mazingira bora ya biashara na uwekezaji, na kuifanya Tanzania kuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji wa kimataifa.
