📌Lengo ni kupunguza foleni, usalama
📌Ni Maelekezo ya Rais Samia
📌Waziri Ulega aagiza manunuzi yaanze mara moja
SERIKALI iko katika hatua za mwisho za kuanza upanuzi wa barabara ya Kitonga mkoani Iringa ambayo sasa itakuwa ya njia nne na yenye taa za barabarani.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kuwa hatua hiyo ni uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan ili kupunguza foleni na kuboresha usalama wa watumiaji barabara katika njia hiyo inayotumiwa na magari mengi.
Waziri Ulega aliyekuwa katika ziara ya ukaguzi wa eneo la zaidi ya kilomita saba linalopaswa kupanuliwa, alisema barabara hiyo ni ya kimkakati kwa uchumi wa nchi kwa sababu inatumiwa pia na magari yanayokwenda katika nchi zinazotumia bandari ya Dar wa Salaam kubeba mizigo yao.
“Barabara hii sasa itakuwa ya njia nne – mbili za kwenda na mbili za kurudi ambapo sasa ni njia mbili tu zinatumika. Na tutafunga taa kote ili kuhakikisha muda wote barabara inapitika muda wote, “ alisema Ulega.
Akitoa picha ya ongezeko la uhitaji wa upanuzi wa barabara hiyo, Mbunge huyo wa Jimbo la Mkuranga alisema idadi ya magari yanayopita katika Barabara Kuu ya TANZAM imeongezeka kutoka magari 1,700 hadi 3,400 kwa siku, hali inayopelekea barabara hiyo kuzidiwa na wingi wa magari.
“Nimepokea mapendekezo kutoka kwa Meneja wa TANROADS Iringa ya kuhakikisha tunaondoa msongamano wa magari katika mlima Kitonga, na nimeelekeza kwa wataalamu wetu kupanua hii barabara kwa kilometa 7. Kwa sasa hivi barabara ina njia mbili kwa hiyo tutatanua na kuwa njia nne”, amesema Ulega.
Waziri Ulega ameongeza kuwa ni maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba kila mradi wa barabara uende sambamba na uwekaji wa taa za barabarani ili kuhakikisha usalama wa watumiaji ikiwemo wananchi, wafanyabiashara na madereva pamoja na kuweka kingo pembezoni mwa barabara ili kuzuia magari yasianguke kwenye makorongo.
“Ninaagiza manunuzi yaanze mara moja ili kuhakikisha kwamba barabara hii inatanuliwa kwani ina umuhimu mkubwa katika uchumi wa nchi hivyo hatuwezi kuiacha katika hali hii na kutimiza pia maelekezo ya Mheshimiwa Rais kutatua changamoto zote”, ameongeza Waziri Ulega.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Ritha Kabati, amesema barabara hiyo ni ya uchumi wa kimataifa hivyo ikitengenezwa itainua zaidi uchumi wa mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla pamoja na kuwasaidia wananchi ambao hupata changamoto ya kufuata huduma za kijamii ikiwemo matibabu Iringa mjini.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS mkoa wa Iringa Eng. Yudas Msangi amesema gharama ya upanuzi wa kilometa 7 wa njia mbili katika barabara hiyo ni bilioni 59.2 na ukarabati wa njia mbili zilizopo ni bilioni 16.2.








