WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imedhamiria kuendelea kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema lengo la Serikali ni kuendelea kuimarisha usalama wa chakula, kupunguza utapiamlo na kuijenga Tanzania yenye wananchi wenye afya bora, nguvu kazi imara na uchumi unaojitegemea.

Amesema hayo leo Alhamisi (Oktoba 16, 2025) wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika Mkoani Tanga, kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Usagara.

“Pamoja na mipango hiyo, Serikali itaendelea kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji, ushirikiano, na ubunifu, ili kuhakikisha nchi inakuwa na chakula cha kutosha kwa matumizi ya ndani na ziada kwa mauzo ya nje”

Amesema kuwa Serikali katika kuhakikisha imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, iliongeza bajeti ya sekta hiyo kutoka shilingi bilioni 246 mwaka 2020/2021 hadi kufikia shilingitrilioni 1.3 mwaka 2024/2025.

“Matokeo ya jitihada hizini dhahiri: uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani milioni 18 mwaka 2020/2021 hadi tani milioni 22 mwaka 2023/2024, huku kiwango cha utoshelevu wa chakula kikiongezeka kutoka asilimia 114 hadi 128 mwaka 2024/2025”.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewasihi vijana nchini wajikite zaidi katika kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa Kwa kuwa sekta ya kilimo ni tegemeo kubwa la ajira. “Serikali imeweka mazingira mazuri ya mikopo, ruzuku, na huduma za ugani ili vijana wawe sehemu ya mapinduzi ya kilimo chenye tija”.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewahimiza wakulima, wafugaji na wavuvi kuhakikisha kuwa baada ya mavuno, waongeze thamani ya mazao kupitia usindikaji na ubunifu, badala ya kuuza mazao ghafi. “Ukiongeza thamani kipato kinakuwa kikubwa zaidi na kinaimarisha usalama wa chakula, na kupunguza upotevu wa mazao unaosababisha hasara kwa wazalishaji.”

Mheshimiwa Majaliwa pia alizipongeza sekta binafsi pamoja na Mashirika ya Kimataifa kwa kuwezesha wakulima wengi kufikiwa na teknolojia za kisasa, mikopo nafuu, na huduma za ugani zilizo bora zaidi. “Ninawashukuru pia wadau wa sekta binafsi, wakiwemo wazalishaji wa pembejeo, viwanda vya usindikaji, taasisi za fedha, na wajasiriamali wadogo, ambao wanashiriki kikamilifu katika kuongeza uzalishaji na kuhakikisha mazao yanapata masoko yenye uhakika”.

kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Mweri amesema kuwa kazi kubwa imefanywa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uwekezaji kwenye sekta ya kilimo iliyowezesha kuifanya nchi kuwa na usalama wa kutosha wa Chakula.

Naye Muwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Suzan Namondo ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyoipiga katika masuala ya kilimo pamoja na usalama wa chakula.

“Kupitia uongozi bora na uwekezaji Tanzania imeongeza kiwango cha uzalishaji wa chakula na kuwezesha nchi hiyo kupiga hatua kubwa katika utoshelevu wa chakula, hii inaonesha namna Tanzania iliyo mchangiaji mkubwa katika usalama wa chakula Afrika Mashariki”

Ameongeza kuwa chakula si suala la uzalishaji pekee, bali linahusu watu na mfumo mzima wa chakula unaounganisha kile tunacholima, namna tunavyokichakata, na iwapo mfumo huo ni mzuri kwa ustawi binadamu pamoja na kulinda mazingira yetu.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Tuungane Pamoja Kupata Chakula Bora Kwa Maisha Bora Ya Baadaye.” ambayo inasisitiza kuwa masuala ya lishe bora, utunzaji wa chakula, na matumizi sahihi ya mazao ya chakula ni jukumu la kila mmoja.