Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli na mafuta mengine ili kuhakikisha bei zake zinaendelea kuwa himilivu, licha ya changamoto za kiusalama za kikanda na kimataifa, ikiwemo za Mashariki ya Kati ambazo zimesababisha kupanda kwa bei ya mafuta nchini.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo, Aprili 01, 2026, wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni, Jijini Dodoma.
“Tumeona bei zimeanza kupanda, hivyo tunataka ndani ya Serikali tuweze kuhakikisha tunakabiliana na hali hiyo ili wananchi waendelee kupata mafuta kwa bei wanazoweza kumudu na kudhibiti ongezeko la gharama za maisha,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kusimamia mifumo ya kuagiza, kuhifadhi na kusambaza mafuta, pamoja na kuongeza uwezo wa kupokea na kuhifadhi mafuta katika Bandari za Dar es Salaam na Mtwara.
Pia ameongeza kuwa Serikali inaendelea na mradi wa ujenzi wa ghala la kuhifadhi mafuta lenye uwezo wa tani 308,110 katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 30.
Dkt. Mwigulu amesema hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha mafuta yanapatikana kwa urahisi, bei zinadumishwa himilivu, na kupunguza athari za mizozo ya kimataifa kwa wananchi.


