Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, ametembelea mradi wa Umwagiliaji uliopo wilayani Masasi mkoani Mtwara ikiwa moja ya muendelezo wa ziara kwa Taasisi za Wizara ya kilimo ambapo amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itakikisha miradi yote ya Umwagiliaji inakamilika na kuleta tija kwa wakulima.
Serikali itahakikisha miradi yote ya Umwagiliaji inakamilika na kuleta tija kwa wakulima hali itakayoimarisha uchumi na kuleta uhakika wa chakula.

Chongolo amesema hayo wakati wa ziara yake katika mradi huo unaotekelezwa eneo la Ndanda, mkoani Mtwara.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa bwawa la Umwagiliaji na uchimbaji wa mifereji mirefu, na ukikamilika unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakulima 700 kutoka vijiji saba.
“Serikali itahakikisha miradi yote ya Umwagiliaji inakamilika na kuleta tija kwa wakulima hali itakayoimarisha uchumi na kuleta uhakika wa chakula, amesisitiza.

Amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa bwawa hilo ambalo litachochea matumaini mapya kwa wakulima wa Mtwara kwa kuwawezesha kulima mazao mbalimbali ikiwemo mboga mboga, mpunga, mahindi na mazao mengineyo.
Ameongeza kuwa ingawa Mtwara inasifika kwa kilimo cha korosho, serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imeanzisha miradi ya Umwagiliaji katika mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuhamasisha uzalishaji wa mazao mengine ndani ya mikoa hiyo bila kutegemea mazao kutoka maeneo mengine.
Aidha, Mhe. Chongolo ameisihi Tume kusimamia kwa umakini miradi hiyo ili kuhakikisha thamani ya fedha iliyowekezwa inaonekana na wakulima wanapata uzalishaji unaoendana na viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) Bw. Raymond Mndolwa, amesema serikali imewekeza na inaendelea kuwekeza fedha nyingi kuhakikisha wananchi wa Lindi na Mtwara wananufaika na miradi ya Umwagiliaji , hatua ambayo itawawezesha kufanya kilimo cha uhakika bila kutegemea mvua.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainabu Telacky amewataka wananchi kushirikiana na Tume katika kulinda miundombinu na rasilimali zilizowekezwa na serikali kwa kuwa wao ndio wanufaika wakuu wa mradi huo.
Akitoa taarifa ya mradi huo ,Mhandisi Macklera Mrutu kutoka Tume amesema kuna jumla ya miradi 26 ya Umwagiliaji katika mikoa ya Lindi na Mtwara yenye thamani ya shilingi bilioni 23.7 Hadi sasa miradi miwili iliyoanza na Utekelezaji ikiwemo ujenzi wa mabwawa na mifereji mirefu , mifereji ya kati ambapo itachukua hekta zaidi ya 300 na utekelezaji wake umefikia asilimia 27%. mpka sasa.

Aidha akiongea kwa upande wa wakulima Bi. Pili Nampokela, wameishukuru serikali kwa kuwafikishia mradi huo wa Umwagiliaji wakisema utawawezesha kulima mara 3 hadi 4 kwa mwaka,na hivyo kuongeza fursa tofauti tofauti kama kuongezeka kwa ajira, kuimarisha usalama wa chakula na kupunguza utegemezi wa mazao kutoka mikoa mingine.






