Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia , Dodoma

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kuanzisha vyanzo vipya vya mapato vitakavyosaidia kudhibiti maambukizi ya UKIMWI pamoja na kugharamia Bima ya Afya kwa Wote, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujitegemea katika ugharamiaji wa huduma muhimu za afya kwa wananchi.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametangaza mpango huo leo tarehe 12 Juni 2025, wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma.

Waziri amesema kuwa hatua hiyo imechochewa na mabadiliko ya kisera duniani ambayo yamesababisha kupungua kwa misaada ya maendeleo, hususan kutoka kwa wahisani wa huduma za afya, hali ambayo imeleta pengo kubwa la kifedha kwenye sekta hiyo.

“Mabadiliko haya yanatulazimu tujipange vizuri kama nchi ili kujitegemea katika kugharamia huduma za afya, hasa kwenye maeneo ya kimkakati kama mapambano dhidi ya UKIMWI na uboreshaji wa bima ya afya kwa wote,” amesema Dkt. Nchemba.

Kwa mujibu wa mpango huo, Serikali inapendekeza kuwa asilimia 70 ya mapato yatakayopatikana kutoka vyanzo hivyo vipya itaelekezwa kwenye Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF), huku asilimia 30 ikielekezwa kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote (NHIF Universal Health Insurance Fund).

Ili kufanikisha hilo, Serikali inapendekeza mabadiliko katika sheria mbalimbali za ushuru na kodi, zikiwemo Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sheria ya Mafuta na Barabara, Sheria ya Madini, Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, na sheria zinazohusiana na usafiri wa umma na uingizaji wa magari na mashine nzito kutoka nje.

Miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kuongezwa kwa ushuru wa bidhaa kwenye vileo: bia (Shilingi 20 kwa lita), mvinyo (Shilingi 30 kwa lita), na pombe kali (Shilingi 50 kwa lita), pamoja na kuongeza ushuru wa huduma za mawasiliano kutoka asilimia 17 hadi 17.5%.

Aidha, Serikali inapendekeza kutoza ushuru wa Shilingi 10 kwa kila lita ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa; ushuru wa asilimia 0.1 kwenye thamani ya soko ya madini; na kuongeza ushuru wa ushindi katika michezo ya kubahatisha kutoka asilimia 10 hadi 15, na kasino za ardhini kutoka asilimia 12 hadi 15.

Kodi nyingine mpya zitahusisha magari yanayoingizwa kutoka nje kulingana na ukubwa wa injini (kuanzia Shilingi 50,000 hadi 200,000), mashine nzito (Shilingi 250,000), pamoja na kodi ya Shilingi 500 kwa tiketi ya treni na Shilingi 1,000 kwa tiketi ya ndege, zitakazotozwa kwa kila abiria.

Dkt. Nchemba amesema kuwa hatua hizo kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Shilingi milioni 586,404.9, na kuongeza kuwa hiyo ni njia ya kujenga mfumo wa kifedha unaojitegemea, wenye uwezo wa kuhudumia wananchi bila kutegemea misaada ya nje.