Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma amesema Serikali itaendelea kuwawezesha vijana katika kuhakikisha wanapata elimu itakayowawezesha kujiajiri na kuajirika.

Akifunga mafunzo ya upambaji wa uso (make up) katika ukumbi wa Baytul Yamiin Bwawani Mjini Unguja, amesema serikali imeamua kufanya hivyo ili kuhakikisha vijana wanapata kujiendeleza kimaisha pamoja na kudumisha utamaduni wa zanzibar.

Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya awamu ya nane imekuwa ikifanya jitihada za kutosha za kuinua kiwango cha ajira kwa vijana katika sekta zisizo rasmin kutokana na uhaba wa fursa katika sekta zilizo rasmi.

Alisema jukumu hilo imekuwa likitekelezwa kwa vitendo kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi kiuchumi ambao wameandaa miongongoni mwa mafunzo hayo kwa kushirikiana na SEBEP.

Riziki aliwapongeza kwa juhudi na kuwa na wazo zuri la kuandaa mafunzo hayo ya kuwawezesha vijana wa kike katika kuwasaidia kuweza kujiajiri na kuajiri kwa lengo la kuindokana na utegemezi.

“Mtaji wa kwanza wa Taifa letu ni watu wake, hivyo mkono wenye ujuzi sio tena kuombaomba bali ni kuweza kujikimu na kuchangia kuendeleza familia na Taifa” alisema Riziki.

Hata hivyo Mhe Riziki amewataka vijana hao kutumia vyema ujuzi walioupata si kwa kujipatia riziki pekee bali pia kuwa mwanga katika jamii kwa kuwafundisha wengine, kuwa mfano wa uadilifu katika biashara yao na kuwapa heshima wateja wao.

Pia Mhe Riziki anetumia fursa hiyo kuwaasa vijana kuendelea kudumisha amani na usalama wakati huu wanapoelekea katika uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi ili kuhakikisha kila mmoja anaendelea kufanya pirika zake za kujipatia kipato.

Naye Mkurugenzi Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) Bw. Juma Burhani Muhammed amesema watahakikisha wanazishawishi taasisi mbalimbali kuweza kuwapatia nafasi za ajira vijana waliopatiwa mafunzo hayo ili kuendeleza ujuzi walioupata.

Kwa upande wake Meneja wa mradi wa kuwajengea uwezo vijana kujiajiri na kuajirika katika uchumi wa Buluu (SEBP) Bw. Salum Mkubwa Abdullah alisema lengo la mradi huo ni kuhakikisha vijana wanapata ujuzi utakaowasaidia kujiinua kiuchumi.

Washiriki wa mafunzo hayo katika risala yao wamesema watahakikisha wanayafanyia kazi mafunzo waliyoyapata kwa kujiajiri na kuchangamkia fursa za ajira zilizopo nchini huku wakimshukuru na kumpongeza mwalimu wao ndugu Emy Broun kwa kuwapa mafunzo hayo yatakayowasaidia kujiari na kuajiriwa.

Jumla ya vijana wanawake 52 wamepatiwa mafunzo ya upambaji wa uso (meke up) yaliyoandaliwa na wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi chini ya mradi wa (sebep) kati yao vijana 10 wamepatiwa ajira na mwalimu wao.