*Mikataba 16 ya Ajira Kimataifa ipo Katika Hatua za Mwisho
Serikali Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano imesaini Mikataba Mitano ambayo itawawezesha wananchi kupata ajira Nje ya Nchi.
Hayo yamesemwa Februari 7, 2026 Jijini Dar es salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu wakati wa Hafla ya Chakula cha Jioni (Gala Dinner) kilichohusisha uzinduzi rasmi wa kipindi cha Imbeju- Bongo Fursa na Jarida la Mapitio ya Vijana lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Biashara na Maendeleo.
“Nlikuwa Falme za Kiarabu nimekutana na Mawaziri wa Kazi kutoka Nchi Mbalimbali na wote walionyesha nia nzuri na nchi yetu, hadi sasa tumesaini Mikataba mitano ambayo iko tayari yamashirikiano na nchi hizi kwa ajili ya Fursa za Ajira kwa Vijana” amesema.
Aidha Mhe. Sangu amesema fursa zilizotajwa kwenye Dira ya Taifa zinapatikana kupitia Wizara hiyo na Serikali inafanya mazungumzo ya mwisho kwenye Mikataba 16 ya Ajira kwa ajili ya Watanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa NEDC, Jesse Madauda Amesema lengo la Jarida na Kipindi chicho ni kuwatia Moyo vijana na Kuwafikia wawekezaji ili waone vijana wa Kitanzania wanafanya shughuli za kibunifu na hatua walizofikia ili iwe rahisi kuwafikia wajasiriamali hao.
Awali akizungumza Mmoja wa Wajasiriamali Elizabeth Consoli ameishukuru serikali kwa kuwa pamoja na wajasiriamali wavumbuzi na kuonyesha nia ya kuwavusha wajasiriamali hao kutoka hatua Moja kwenda Hatua nyengine.







