Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe profesa Adolf Mkenda amesema serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika Wilaya 64 nchini.

Waziri Mkenda amesema hayo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika kipindi cha miaka minne.

Waziri Mkenda amesema kuwa ujenzi wa vyuo hivyo ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata fursa za mafunzo ya Ufundi Stadi.

Waziri Mkenda amesema kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aliagiza fedha zitolewe ili kukamilisha ujenzi wa vyuo vya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ambavyo hazijakamilika ili zianze kufanya kazi haraka.

Amesema kuwa kwa Tanzania Bara kila mkoa utakuwa na VETA yenye hadhi ya mkoa hivyo kazi ya Wizara yake ni kuzitengeneza hizo VETA ili ziweze kutoa watu ambao wana ujuzi na uwezo wa kufanya kazi ndani na nje ya nchi.