Serikali kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kuendelea kufungua milango zaidi ya uwekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa za afya na kupanua soko ndani na nje ya Tanzania.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, Novemba 19, 2025 jijini Dodoma, alipokutana na uongozi wa Taasisi ya Shandong Hongyu Medical Technology Group kutoka China, waliowasilisha dhamira ya kuwekeza kiwanda cha dawa na vifaa tiba nchini.

Waziri Mchengerwa alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuona uwekezaji wa viwanda hivyo unaongezeka na wawekezaji wanapewa kipaumbele katika mchakato wa kuwekeza na kupata masoko.

“Kama kweli wamedhamiria kuwekeza Dola Milioni 500, Serikali haiwezi kuacha uwekezaji huu. Tutapima umakini wao na dhamira yao kupitia maombi yao watakayoyaleta. Nawaelekeza Mfamasia Mkuu na Katibu Mkuu kukaa na wawekezaji hawa, kuwapa miongozo ya Serikali na kuhakikisha wanaondoka hapa wakiwa na uhakika kuwa Serikali imedhamiria kufanya nao biashara na kuwapa masoko ya ndani na nje, iwapo wataweza kuzalisha kwa kiwango kinachotakiwa. Jambo hili likamilike leo,” alisema Mchengerwa.

Aidha, alisisitiza kuwa hakuna sababu ya kuwazuia wawekezaji wanaokidhi vigezo, kwakuwa ardhi ya ujenzi na masoko yanapatikana, hivyo Serikali itaendelea kuwakaribisha ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya kwa urahisi.

“Wanapokwenda kujenga viwanda, halmashauri zitapata mapato kutokana na kodi. Kwa hiyo wawekezaji wa viwanda vya bidhaa za afya wapokewe na kupewa nafasi. Wakija Watanzania ni vizuri zaidi, lakini hata wakitoka nje tutawakaribisha,” aliongeza.