Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali ya Mkoa wa Mwanza imeanza kuchukua hatua madhubuti kudhibiti ongezeko la shughuli za uchimbaji wa madini kiholela katika maeneo ya Kasandi na Ishokela Hela, yaliyopo Wilaya ya Misungwi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha rasilimali hizo zinaleta manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema kuwa sekta ya madini kwa sasa imekuwa kichocheo kikuu cha uchumi kwa mkoa huo, hivyo ni lazima shughuli zake zifanyike kwa kufuata sheria, kuzingatia usalama wa wachimbaji na kulinda mazingira.
“Tumeona ongezeko la wachimbaji wadogo katika maeneo kama Kasandi na Ishokela Hela. Tunatambua umuhimu wa madini haya kwa wananchi wetu, lakini hatuwezi kuruhusu shughuli za kiholela zisizozingatia sheria, usalama, wala ustawi wa jamii. Ndiyo maana tumechukua hatua za kuhakikisha utaratibu unakuwepo,” amesema Mtanda
Ameeleza kuwa moja ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwatuma maafisa kutoka Ofisi ya Afisa Madini wa Mkoa (RMO) kwa ajili ya kufanya utambuzi wa maeneo yenye shughuli za uchimbaji, kuwatambua wachimbaji na kuwasaidia kujiunga katika vikundi rasmi vinavyotambulika kisheria.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, wachimbaji hao pia wameanza kupewa mafunzo ya kitaalam juu ya usalama, uhifadhi wa mazingira, na mbinu bora za uchimbaji wa kisasa, ili kuwajengea uwezo wa kufanya kazi zao kwa tija na kwa usalama zaidi.
“Wachimbaji wengi wa awali walikuwa hawana uelewa wa sheria wala mbinu bora za uchimbaji. Tumeanza kuwaelimisha na kuwasajili rasmi ili waweze kufaidika na mikopo, masoko na usimamizi wa kitaalam. Tumejipanga kuhakikisha madini haya yanawanufaisha wananchi badala ya kuwa chanzo cha migogoro,” ameongeza.
Katika kuhakikisha uchimbaji holela unakomeshwa, Serikali ya Mkoa pia imetangaza kutumia kikosi kazi maalum cha ufuatiliaji (RUSH – Rapid Unit for Safety and Harmony) kinachopelekwa haraka pindi dalili za uchimbaji haramu zinapojitokeza katika maeneo mbalimbali.
Aidha, ameeleza kuwa Mkoa wa Mwanza uko kwenye maandalizi ya kupokea uwekezaji mkubwa kupitia mgodi wa kimataifa wa Nyanzaga, ambao unatarajiwa kuwa miongoni mwa migodi mikubwa ya dhahabu nchini, hatua inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa wakazi wa mkoa huo.
“Mradi wa Nyanzaga ni tumaini jipya kwa wananchi wa Mwanza. Tunataka jamii nzima iishi kwenye madini haya, si kwa kuishia kuwa watazamaji bali kwa kuwa washiriki wakuu katika mnyororo wa thamani wa madini. Tunalenga kuwabadilisha wachimbaji wadogo kuwa wafanyabiashara wa kweli wa madini,” amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.

Aidhaa ameeleza kuwa Mkoa umeweka wazi kuwa itaendelea kushirikiana na Wizara ya Madini na taasisi nyingine za udhibiti ili kuhakikisha shughuli zote za madini zinachangia kwa ufanisi katika maendeleo ya jamii na uchumi wa Taifa, huku wananchi wakipewa nafasi ya kushiriki kikamilifu na kunufaika kwa njia ya moja kwa moja.
