πŸ“ Mapama, Arumeru – Arusha

Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na wadau wa mazingira na maji, imezindua rasmi zoezi endelevu la upandaji miti katika Skimu ya Umwagiliaji Mapama.

lengo la jitihada hizo za pamoja ni kulinda vyanzo vya maji, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika kwa shughuli za kilimo.

Akizindua zoezi hilo, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Afisa Tarafa wa Mbuguni, Deogratius Msuha, amewakumbusha wananchi kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mmoja.

Ameeleza kuwa kupanda miti pekee haitoshi bila kushirikiana katika kuitunza na kusimamia ili ilete matokeo yaliyokusudiwa.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuzingatia sheria za utunzaji wa mazingira kwa kuheshimu mipaka ya mito, ikiwemo kutolima au kufanya shughuli za kijamii ndani ya mita sitini kwa pande zote za kingo za mito, pamoja na kutoa taarifa kwa uongozi pale wanapoona uharibifu wa vyanzo vya maji.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Arusha, William Simon, amesema zoezi hilo limezingatia umuhimu wa Mto Kikuletwa ambao ni mto pekee unaotegemewa na skimu nyingi za umwagiliaji katika eneo hilo.

Amesema upatikanaji wa maji lazima uende sambamba na utunzaji wa mazingira ili kuendeleza kilimo cha uhakika.

Amefafanua kuwa uharibifu wa vyanzo vya maji unasababishwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za binadamu ikiwemo kilimo kwenye vyanzo vya maji na ukataji miti, hali inayochangia mmomonyoko wa udongo na kuathiri miundombinu ya umwagiliaji.Ameongeza kuwa endapo mazingira hayatatunzwa, uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika miundombinu ya Umwagiliaji utakuwa hauna tija.

Aidha, Mjairi Baraka ambaye ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru na Mhandisi wa Umwagiliaji, Halimashauri ya Wilaya ya Meru , amesisitiza umuhimu wa kuuona mto kama sehemu ya maisha ya wananchi, akibainisha kuwa bila mto huo shughuli za kilimo na maisha ya jamii yatayumba.

Amehimiza usimamizi bora wa kingo za mto kwa mujibu wa sheria za mazingira.

Katika zoezi hilo, jumla ya miti 8,000 inapandwa kando ya Mto Kikuletwa katika Skimu ya Mapama, huku viongozi wakieleza kuwa zoezi hilo ni endelevu na litaendelea hadi maeneo mengine.

Viongozi wa skimu wametakiwa kuweka ratiba maalum za upandaji na usimamizi wa miti katika kila ukanda.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Mkulima wa Skimu ya Mapama, Harrison Tobias, amesema upandaji wa miti utasaidia kulinda vyanzo vya maji na kuongeza uhakika wa maji kwa kilimo.

Amesema wakulima wako tayari kushirikiana na serikali katika kutunza mazingira ili kunufaika na miradi ya Umwagiliaji na kuboresha uzalishaji kupitia kilimo cha Umwagiliaji katika eneo hilo.

Skimu ya Umwagiliaji Mapama inanufaisha vijiji vya Majengo, Pakanundo na Makiba, na zoezi la uzinduzi wa upandaji miti linatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha utunzaji wa mazingira na maendeleo endelevu ya kilimo katika eneo hilo.

Aidha zoezi hilo la upandaji miti limehusisha wadau mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Bodi ya Maji Bonde la Pangani pamoja na Wakala wa Misitu nchini TFS.