Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuenzi na kudumisha mchango mkubwa wa kimaendeleo ulioachwa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Job Yustino Ndugai.

Akizungumza katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma mara baada ya ibada maalumu ya kuuaga mwili wa marehemu, Rais Samia amesema Ndugai alikuwa miongoni mwa viongozi waliopambana kuhakikisha vijana wanapata elimu bora, na kwamba kifo chake kimeacha pengo kubwa, hususan kwa vijana wa Jimbo la Kongwa alikolitumikia kwa muda mrefu.

“Pamoja na mambo mengi mazuri aliyoyafanya, ukweli ni kwamba kifo ni njia ya kila mwanadamu,tunamuomba Mungu aendelee kuipa faraja familia yake na kuwaongoza katika kipindi hiki kigumu,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema Ndugai ameacha alama tatu muhimu katika mkoa huu ambazo ni kuimarisha nidhamu ya vikao na kuhimiza maendeleo, kufanya mapinduzi ya elimu katika mkoa mzima na wilayani Kondoa, pamoja na kuhamasisha zao la korosho katika wilaya za Kongwa na Mpwapwa.

Awali, Katibu wa Bunge, Baraka Leonard, akisoma wasifu wa marehemu, ameeleza kuwa Ndugai alifariki dunia Agosti 6, 2025, saa 9 alasiri jijini Dodoma, kutokana na shinikizo la damu kushuka sana (septic shock) lililosababishwa na maambukizi makali ya mfumo wa hewa (severe pneumonia).

Marehemu amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanzania Wildlife Protection Fund (2001–2004), Mjumbe wa Bodi ya Hifadhi ya Ngorongoro (2007–2010), Mjumbe wa Baraza la Seneti la Chuo Kikuu cha Dodoma (2007–2010), na Mjumbe wa Bodi ya Uwekezaji ya Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika (2015–2022).

Aidha, amekuwa muumini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mzee wa Kanisa, na hadi umauti unamkuta alikuwa Lay Canon wa Dayosisi ya Mpwapwa — nafasi muhimu ya kumshauri Askofu.

Ndugai alizaliwa Januari 21, 1963, katika Kijiji cha Laikala, Kata ya Sagara, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, na amefariki akiwa na umri wa miaka 65. Ameacha mke, watoto na wajukuu.