Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Iringa

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa trilioni 1.2 kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa kwa lengo la kubiresha miradi ya umwagiliaji nchini.

Hayo yamebainishwa leo Juni 24, 2925 na Mkurugenzi wa NIRC, Raymond Mndolwa wakati semina iliyoshirikisha wahariri kutoka vyombo mballimbali vya habari mkoani Iringa ambapo alisema Serikali imeisaidia kwa kiwango cha juu na kuchangia tume hiyo kupata miradi ya umwagiliaji mipya.

Amesema fedha hizo zimefanikisha na kuimarisha usimamizi wa shughuli za umwagiliaji nchini.

Amesema katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi, tume itahakikisha upatikanaji wa maji kwa matumizi ya kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga mabwawa, kuchimba visima na ujenzi wa miundombinu katika mabonde 22 ya kimkakati pamoja na kuanza matumizi . kutoka ziwa Victoria na Tanganyika.

Hata hivyo katika mkutano huo Mndolwa ametaja mafanikio ya tume hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015 hadi 2025 yametokana na kuongezeka kwa bajeti kutoka sh.bilioni 51.49 kwa mwaka 2021/2022 hadi sh.bilioni 403.78 mwaka 2024/2025 sawa na asilimia 684.19.

Mndolwa ametaja mafanikio mengine ni ongezeko la eneo linalomwagiliwa kutoka hekta 461,000 mwaka 2014/2025 hadi hekta 983,466.06 mwaka 2024/2025.

Aidha Mndolwa ametaja matarajio ya sekta ya umwagiliaji nchini ambayo ni kuongeza eneo linalomwagiliwa kutoka hekta 983,466.6 mwaka 2025 hadi hekta 5,000,000 ifikapo mwaka 2030.

Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa tija katika uzalishaji wa mazao mbalimbali katika skimu zote za umwagiliaji nchini.

“Matatajio yetu mengine ni kuongezeka kwa ajira na kipato cha mkulima mmoja mmoja na kuongezeka kwa mchango wa kilimo cha umwagiliaji katika pato la taifa,”amesema.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Nchini (TEF), Deodatus Balile aliipongeza tume hiyo kwa maendeleo yaliyopatikana katika vipindi mbalimbali na kuhakikisha kilimo kinasonga mbele.

“Mmefanya jitihada nyingi na nzuri huku mkihakikisha Tanzania haitakuwa na upungufu wa chakula,”alisema.

Pia kutokana na juhudi hizo zitasaidia pato la mkulima kuongezeka kupitia kilimo cha umwagiliaji ambacho tayati fursa zimeanza kuonekana.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake( TAMWA), Joyce Shebe alisema kuwepo kwa kilimo cha umwagiliaji kimesaidia jamii kupata chakula katika msimu wote na kuacha kutegemea mvua za msimu.

“Kilimo cha umwagiliaji kimekuwa mkombozi kwa mkulima kwa sababu wakati wote mkulima anakuwa yupo katika mzunguko wa kilimo kwa kulima mazao ya yenye tija kwa taifa,”alisema.