Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza ahadi za Rais Samia kwa vitendo, hususan katika kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanajisikia kuwa sehemu ya jamii na hawatengeki na wanafunzi wengine.

‎Akizungumza na waandishi wa Habari Januari 31, 2026 katika Ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo jijini Dodoma, katika kutoa taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Rais samia ndani ya siku 100.

‎amesema kuwa Wizara imenunua na kusambaza vifaa vya kidijiti na saidizi vyenye thamani ya shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya walimu wa shule za msingi na sekondari, wakufunzi pamoja na walimu tarajali wenye ulemavu katika vyuo vya ualimu nchini, kwa lengo la kurahisisha ujifunzaji na ufundishaji.

‎Amebainisha kuwa jumla ya wanufaika 1,055 kutoka Halmashauri 104 nchini wamenufaika na mpango huo. Amesema kuwa vifaa vilivyosambazwa ni pamoja na kompyuta mpakato 680, Brain Note Touch Pass 9, voice recorder 377, tablets 196 kwa ajili ya wanaotumia lugha ya alama, mashine za Perkins Braille 30, vifaa vya kusaidia kusikia 101 pamoja na mashine za Everest Drill Embosser.

‎Pia ameongeza kuwa mashine hizo zinawezesha walimu wasioona kuchapa maandishi kwa kutumia nukta nundu na hatimaye kuchapisha maandishi ya kawaida yanayoweza kusomwa na wanafunzi wengine.

‎Amesema kuwa hatua hiyo ni muendelezo wa juhudi zilizoanza katika Serikali ya Awamu ya Sita, na akaeleza kuwa kila mwaka Serikali imekuwa ikigawa vifaa vya kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na vitabu vinavyochapishwa na Serikali kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita.

‎Aidha amebainisha kuwa kila kitabu kinachotolewa kinakuwa na nakala maalum kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, ikiwemo vitabu vyenye maandishi makubwa kwa wenye uoni hafifu na vitabu vya nukta nundu (Braille) kwa wasioona kabisa, vinavyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).

‎Pia ameongeza kuwa utekelezaji wa ahadi za Rais unaenda sambamba na upanuzi wa fursa za elimu kupitia utoaji wa mikopo na ujenzi wa miundombinu ya elimu ya juu, ambapo amesema kuwa Tanzania inaendelea kujenga kampasi mpya 16 za vyuo vikuu katika mikoa ambayo awali haikuwa na kampasi hizo.

‎Amebainisha kuwa mikoa yote nchini tayari ina vituo vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, huku ujenzi wa kampasi mpya ukiendelea katika maeneo mbalimbali ikiwemo kampasi ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) mkoani Kigoma na Kagera pamoja na kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mkoani Lindi, ambapo jiwe la msingi tayari limewekwa.