Serikali ya Tanzania imeahidi kuendelea kuwekeza kwa nguvu katika miundombinu ya usafiri kwa lengo la kukuza biashara na kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia Ukanda wa Kati, huku viongozi wa nchi wanachama wakiahidi kushirikiana kwa karibu ili kuinua maendeleo ya kiuchumi katika ukanda huo muhimu wa usafirishaji.

Akizungumza katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Usafirishaji wa Ukanda wa Kati (CCTTFA), uliofanyika jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa, ameeleza kuwa serikali yake imejipanga kuendeleza miradi mikubwa ya reli, bandari na usafiri wa majini na anga, ili kuongeza ufanisi na ushindani wa Ukanda wa Kati katika soko la kikanda na kimataifa.

Prof. Mbarawa amesema kuwa huduma za abiria za reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) kati ya Dar es Salaam na Dodoma zimekuwa na mafanikio makubwa, na sasa serikali inaelekea kuanzisha huduma za mizigo mwezi Julai mwaka huu. Tayari mabehewa 264 kati ya 1,430 yaliyopangwa yamewasili nchini, jambo linalotoa matumaini kwa sekta ya usafirishaji wa mizigo kuelekea katika ushindani wa kimataifa.

Katika kuboresha usafiri wa reli wa kikanda, Prof. Mbarawa alieleza kuwa Tanzania, Zambia na China ziko katika hatua za mwisho za kufufua Shirika la Reli la TAZARA, ambapo uwezo wa reli hiyo utapandishwa hadi tani milioni 2.4 kwa mwaka, kutoka tani 400,000 za sasa.

Akieleza kuhusu maboresho ya bandari, Prof. Mbarawa amesema kuwa uwekezaji wa kampuni za kimataifa kama DP World na Adani Group umeongeza ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam, huku serikali ikiendelea kuboresha miundombinu ya reli inayounganisha bandari hiyo kwa lengo la kupunguza msongamano na kuongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo.

Katika upande wa usafiri wa majini, serikali inatekeleza miradi katika maziwa makuu ikiwemo ukarabati wa meli za MV Liemba na MV Mwongozo katika Ziwa Tanganyika, pamoja na ujenzi wa meli mpya za mizigo na abiria. Katika Ziwa Victoria, ujenzi wa meli mpya ya MV New Mwanza na ukarabati wa MT Ukerewe na MT Nyangumi unaendelea.

Mkutano huo pia uliidhinisha ujenzi wa jengo jipya la makao makuu ya CCTTFA jijini Dar es Salaam, ghorofa nane ambalo linatarajiwa kuanza kujengwa mwaka ujao wa fedha. “Uamuzi huu unaonyesha dhamira ya pamoja ya nchi wanachama kuendeleza ushoroba huu kwa faida ya wananchi wake,” alisema Prof. Mbarawa.

Waziri wa Uchukuzi wa Zambia, Frank Tayali, alieleza kuwa Zambia, kama nchi isiyo na bandari, inategemea mno miundombinu ya nchi jirani kwa usafirishaji wa bidhaa. “Gharama za usafirishaji bado ni kubwa kwa uchumi wetu, hivyo juhudi hizi za kuboresha reli na bandari ni muhimu sana kwetu,” alisema Tayali.

Katika mkutano huo, Malawi ilikabidhiwa rasmi nafasi ya Uenyekiti wa CCTTFA kutoka kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Waziri wa Uchukuzi wa Malawi, Mhandisi Jacob Hara, amesema katika kipindi cha uongozi wake atahakikisha kuna msisitizo mkubwa katika miradi ya usafiri, ikiwemo ujenzi wa makao makuu mapya ya CCTTFA.

Katika hatua ya kuimarisha ushirikiano, Tanzania na DRC zilikabidhiana hati za maeneo kwa ajili ya ujenzi wa bandari kavu. Tanzania ilikabidhi maeneo ya Kwara na Katosho kwa DRC, huku DRC ikikabidhi eneo la Kasumbaresha kwa Tanzania, hatua inayoashiria mshikamano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.