Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kuwawezesha wananchi kupata hati milki za ardhi ili kuongeza kasi ya umilikishaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Uwezeshaji huo unafanyika kupitia mazoezi ya urasimishaji makazi holela pamoja na Kliniki Maalum za Ardhi zinazofanyika maeneo mbalimbali nchini zikiwa na lengo la kuongeza kasi ya umilikishaji ardhi na kusogeza huduma karibu na wananchi.

Kwa upande wa mkoa wa Arusha inapofanyika Kliniki ya Ardhi katika kata ya Muriet, jumla ya viwanja 18,886 vimetambuliwa na viwanja 14,562 vimeidhinishwa.

Akizungumza wakati wa kliniki hiyo tarehe 16 Oktoba 2025 jijini Arusha, Mratibu wa Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha (KKK) Bw. Elia Kamihanda amesema, kliniki hiyo ya ardhi mbali na kutoa huduma mbalimbali za sekta ya ardhi inatilia mkazo kuongeza kasi ya umilikishaji ardhi hususan kwa wanannchi waliorasimishiwa makazi yao katika kata ya Muriet.

“Huduma hii ya kliniki ya ardhi ina manufaa makubwa hususan kwa wananchi wa Muriet waliorasimishiwa maeneo yao kwa kuwa watapata usalama wa milki yao na kuweza kusimamia haki zao kupitia nyaraka za milki’’ amesema Kamihanda.

Amewataka wananchi wa Muriet kujitokeza kwa wingi katika kliniki hiyo ya Ardhi ili waweze kupata huduma za sekta ya ardhi sambamba na kumilikishwa maeneo yao kwa kupatiwa hati alizozieleza kuwa, zitawasaidia katika shughuli zao za kimaendeleo pamoja na kuepuka migogoro ya ardhi.

Maeneo ambayo kliniki hizo maalum za ardhi zinafanyika nchini ni Chalinze mkoa wa Pwani, Nzega Tabora, Mbarali Mbeya pamoja na wilaya ya Njombe mkoa wa Njombe. Huduma hizo zinatarajia pia kuendelea katika halmashauri ya manispaa ya Mtwara Mikindani na Peramiho, Ruvuma.

Huduma zinazotolewa kupitia Kliniki hizo Maalum za Ardhi ni utoaji hati milki za ardhi papo kwa hapo kwa waliokamilisha taratibu za umiliki, utoaji elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mfumo wa utoaji huduma za ardhi kidigiti (e-ardhi) na usaidizi wa ufunguaji akaunti ya mwananchi katika mfumo wa e-ardhi.

Huduma nyingine ni uhakiki na utambuzi wa viwanja vya wananchi uwandani, utoaji namba ya malipo (control number) za ada mbalimbali za serikali kwa ajili ya umilikishaji pamoja na kupokea, kusikiliza na kutatua migogoro za ardhi kiutawala.