Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

SERIKALI imesisitiza azma yake ya kuendelea kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kuchochea ukuaji wa sekta za viwanda, kuongeza fursa za ajira, na kukuza mchango wa kiuchumi wa sekta binafsi.

Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa viwanda vya ndani vinazalisha kwa tija, vinatumia teknolojia ya kisasa, na bidhaa zake zinatambulika kimataifa kwa ubora na viwango vinavyostahili ili kuleta ushindani wa kweli katika soko la ndani na nje.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kampuni za Huawei, Sunflag (Tanzania) Limited, GS1 Tanzania, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), pamoja na Kampuni ya Saruji ya Dangote 17 Machi 2026 jijini Dodoma.

Akiwa aliambatana na Naibu Katibu Mkuu Bw. Aristides Mbwasi, katika vikao hivyo, Waziri. Kapinga amebainisha kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara binge za kisekta imejipanga kutatua changamoto za Wafanyabiashara na Wawekezaji ili kuchochea mapinduzi ya viwanda nchini.

Katika mazungumzo yake na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Biashara wa Huawei, Bw. Vicent Wen, pande zote mbili zimejadili namna ya kuimarisha ushirikiano kupitia TEHAMA ili kuzalisha ajira na kukuza ubunifu wa kidijitali kupitia programu za DigiTruck na ICT Academy.

Vilevile, alikutana na Kaimu Mtendaji Mkuu wa kiwanda cha nguo cha Sunflag (Tanzania) Limited, Bw. Emmanuel Mwabuka, na kumhimiza kuweka lebo ya “Made in Tanzania”ili kutangaza ubora wa bidhaa za ndani na kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa malighafi ya pamba.

Kuhusu Sekta ya Saruji, Waziri amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Saruji ya Dangotenchini Tanzania, Bw. Adeyemi Fajobi, na kusitiza kuwa Serikali itaendelea kusaidia viwanda vya kampuni hiyo vilivyopo Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, na Tanga.

Mazungumzo hayo yamejikita katika mikakati ya kuongeza uzalishaji, kuhakikisha upatikanaji wa malighafi muhimu na rasilimali nyingine ili kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta hiyo ambayo ni nguzo ya ujenzi wa miundombinu.

Wizara pia imepiga hatua katika biashara ya kidijitali kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa GS1 Tanzania, Bi. Fatuma Kange, katika utekelezaji wa Mpango wa Sunrise 2027.

Mpango huu unalenga kuhama kutoka matumizi ya 1D barcodes kwenda 2D barcodes kama QR codes ifikapo mwaka 2027, mabadiliko yatakayowezesha bidhaa za Tanzania kubeba taarifa nyingi zaidi, kuboresha ufuatiliaji wa bidhaa sokoni, na kuongeza uwazi na ushindani katika mnyororo wa ugavi wa kimataifa.

Aidha, Waziri Kapinga amekutana na Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Bw. Emmanuel Kyarwenda, na kuipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji wake endelevu katika viwanda vya Moshi, Dar es Salaam, na Mwanza. SBL imetoa ajira rasmi kwa zaidi ya watu 800 na kunufaisha wengine 140,000 kupitia mnyororo wake wa thamani, jambo linaloonesha mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kuongeza thamani ya bidhaa za ndani na kuimarisha mitandao ya ugavi wa ndani.

Vilevile Waziri Kapinga alisema kuwa Serikali inathamini michango ya viongozi hawa na makampuni yao katika kukuza viwanda mama na kutengeneza fursa za kiuchumi kwa Watanzania, huku akisisitiza kuwa ukuaji huu lazima uende sambamba na utambulisho wa bidhaa za Kitanzania duniani.