Michezo ya kubahatisha imeingiza serikalini kiasi cha Sh Bil.17.42 kwa mwaka wa fedha 2024/25, huku ikipanga kukusanya Sh Bil.29.89 kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Kauli hiyo imetolewa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alipokuwa akiwasilisha mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/25 na mapendekezo ya mpango na bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/26.
“Kwa mwaka 2024/25, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania ilipanga kutoa leseni 12,456 ikijumuisha leseni mpya 1,126 na kuhuisha leseni 11,330; kufanya kaguzi 12 kwa kuzingatia vihatarishi; kutekeleza operesheni nne (4) za kudhibiti michezo haramu ya kubahatisha.
“Kukusanya mapato yatokanayo na michezo ya kubahatisha ya jumla ya shilingi bilioni 24.89; kuendelea kuelimisha jamii kuhusu athari hasi za michezo ya kubahatisha; na kusimamia uendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa.
“Hadi Aprili 2025, Bodi imetoa leseni 8,466, sawa na 47 asilimia 67.9 ya lengo ikijumuisha leseni mpya 2,008 na zilizohuishwa 6,458; kufanya kaguzi tisa (9) katika michezo ya kasino, kubashiri matokeo na mashine dubwi (Slot Machines), sawa na asilimia 75 ya lengo; na kufanya operesheni tatu (3) za kudhibiti michezo haramu ya kubahatisha, sawa na asilimia 75 ya lengo.
“Aidha, Bodi imekusanya jumla ya shilingi bilioni 17.42, sawa na asilimia 70 ya lengo la mwaka na kufanya programu tatu (3) za kuelimisha jamii juu ya michezo ya kubahatisha, faida na hasara pamoja na dhana nzima ya kucheza kwa kiasi (responsible gaming),” amesema.
