Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Serikali imesema itaendelea na jitihada zake za kukuza sekta ya horticulture kama injini muhimu ya mageuzi ya kiuchumi, ajira, kipato na mauzo ya nje.

Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 12,2025 Jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Jim Yonazi, kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, wakati akifungua Mkutano wa Biashara na Uwekezaji wa Horticulture (HoBIS2025).

Dk. Yonazi amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imefanya mageuzi makubwa ya kimuundo na kisera yaliyolenga kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuongeza ushindani wa kimataifa wa mazao ya horticulture. Alibainisha kuwa kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) ni miongoni mwa hatua zilizosaidia kurahisisha usimamizi na maendeleo ya sekta hiyo.

Aidha, amesema Serikali imeboresha sera za kodi na biashara, kuimarisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), na kujenga miundombinu muhimu kama umwagiliaji, maghala ya baridi, vituo vya ukaguzi wa viwango, pamoja na maboresho katika viwanja vya ndege na bandari kuu za nchi ambapo hatua hizo, zimeongeza ufanisi wa uzalishaji na usafirishaji wa mazao ya horticulture kwenda masoko ya kimataifa.

Akizungumzia uhusiano wa sekta hiyo na mipango ya taifa, Dk. Yonazi amesema juhudi hizo zinaendana na Mpango Mkuu wa Kilimo 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III), ambapo horticulture imepewa kipaumbele kama kichocheo cha ajira na ukuaji wa viwanda vya kusindika mazao.

Amewataka wadau wa sekta hiyo kushirikiana kwa vitendo katika kukuza ubora wa bidhaa na kufuata viwango vya kimataifa ili Tanzania iweze kushindana kimataifa kwa ubora na uaminifu, na si bei pekee.

“Soko la dunia linabadilika kwa kasi. Ni lazima tuwe wabunifu, wenye ubora na wenye kuaminika,” amesisitiza.

Kwa upande wa mipango ya baadaye, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya umwagiliaji, masoko ya ndani, bandari na viwanja vya ndege. Aidha, Serikali kupitia Tume ya Rais ya Mageuzi ya Kodi, inaendelea kuboresha sera za kifedha ili kuimarisha uwekezaji na urahisi wa kufanya biashara katika sekta ya kilimo. Alihitimisha kwa kusema, “HoBIS2025 si jukwaa la mijadala tu, bali ni jukwaa la utekelezaji na Serikali iko tayari kusimamia matokeo yake.”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, amesema sekta ya horticulture imekua kwa kasi kubwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka tani milioni 1.1 mwaka 2003/04 hadi tani milioni 8.4 mwaka 2024, na mapato ya mauzo nje kuongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 64 hadi milioni 569.

Amesema mafanikio hayo yametokana na sera madhubuti za serikali, uwekezaji wa kimkakati na ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

“horticulture sasa imepewa kipaumbele katika mipango ya kitaifa kama ASDP II, Agenda 10/30, na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano”,Amesema.

Aidha amewataka wadau wote kutumia HoBIS 2025 kama jukwaa la kuweka mikakati ya pamoja itakayohakikisha sekta ya horticulture inakuwa chachu ya uchumi jumuishi, ubunifu na maendeleo endelevu kwa Watanzania wote.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wakulima wa Horticulture Tanzania (TAHA), Dkt. Jacqueline Mkindi, amesema kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu la kujenga ushirikiano, kubadilishana ujuzi na kuibua fursa za uwekezaji zitakazochochea ushindani wa sekta hiyo.

Mkutano wa Biashara na Uwekezaji katika Sekta ya Horticulture (HoBIS 2025) umefunguliwa rasmi jijini Dar es salaa na kukutanisha wadau, wawekezaji, watafiti, watunga sera na viongozi wa sekta binafsi kujadili mustakabali wa ukuaji endelevu wa kilimo cha mboga, matunda na maua nchini.