Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali imetoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vya kutengeneza vifaa tiba na dawa kwa ajili ya matibabu ya maradhi ya afya ya kinywa na meno, ili kuimarisha huduma za afya na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya ya Kinywa kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Baraka Nzobo, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati wa kufunga maonesho ya siku mbili ya bidhaa na huduma za afya ya kinywa na meno (Tanzania Dental Expo), yaliyofanyika Mei 30 na 31, jijini Dar es Salaam.

“Kwa kupitia maonesho haya, napenda kuwakaribisha wawekezaji wa huduma za afya ya kinywa na meno kuchangamkia fursa zilizopo hapa nchini kwa kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa na vifaa tiba vya afya ya kinywa na meno,” alisema Dkt. Nzobo.
Dkt. Nzobo alibainisha kuwa jiografia ya Tanzania inaiweka nchi katika nafasi ya kipekee ya kibiashara, kwani viwanda vitakavyoanzishwa vitahudumia si tu soko la ndani bali pia nchi jirani, hivyo kuongeza pato la taifa na kutoa ajira kwa Watanzania.
“Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau wote wa sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora. Ushiriki wetu katika maonesho haya ni ushahidi wa dhamira hiyo,” aliongeza Dkt. Nzobo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzania Dental Expo, Dkt. Ambege Mwakatobe, alisema lengo la kuandaa maonesho hayo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa kuwa yamewakutanisha wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na watoa huduma, watengenezaji wa vifaa tiba na wananchi kwa ujumla.
“Maonesho haya yamekuwa chachu ya maendeleo kwa wanataaluma wa afya ya kinywa na meno. Wamejifunza, wamebadilishana uzoefu na kuona teknolojia mpya zitakazowasaidia kuboresha huduma wanazotoa,” alisema Dkt. Mwakatobe.
Aidha, aliwahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kuchunguza afya ya kinywa na meno mara kwa mara ili kuweza kugundua mapema matatizo yoyote yanayoweza kujitokeza.
Dkt. Mwakatobe pia alieleza kuwa, licha ya kuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuandaa maonesho kama hayo, wataalamu wengi wameonyesha furaha na hamasa ya kushiriki tena katika miaka ijayo kutokana na manufaa waliyoyapata.
Dkt. Aloyce John kutoka Mwanza, mmoja wa washiriki wa maonesho, alisema maonesho hayo yamewapa motisha kubwa ya kuendelea kujifunza, hasa kutokana na uwepo wa vifaa vya kisasa vinavyohitaji ujuzi wa ziada ili kuvitumia kwa ufanisi.
“Matatizo ya afya ya kinywa na meno yanaongezeka kwa kasi nchini kutokana na ukosefu wa elimu sahihi juu ya usafi wa kinywa na ulaji wa vyakula vinavyoharibu meno. Tunahitaji kuongeza juhudi katika kutoa elimu hiyo,” alisema Dkt. Aloyce.

Naye mwanafunzi wa fani ya afya ya kinywa kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Bw. Boaz Nkono, alisema maonesho hayo yamewapa picha halisi ya changamoto na fursa zilizopo katika sekta hiyo.
“Awali nilidhani fursa ni kuajiriwa tu, lakini kupitia maonesho haya nimegundua kuwa ninaweza kujiajiri na hata kuwaajiri wengine. Hii ni fursa ya kipekee kwa sisi vijana,” alisema Bw. Nkono.
