Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za haraka katika kuimarisha usalama barabarani kwa kuboresha usanifu wa miundombinu, kuimarisha utekelezaji wa sheria, pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu ili juhudi hizo ziweze kuleta matokeo chanya kwa watumiaji wote wa barabara.
Dkt. Msonde ametoa kauli hiyo Mkoani Dodoma Februari 25, 2026, wakati akifungua mafunzo ya ukaguzi wa usalama barabarani yaliyoandaliwa na Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Lund kutoka Sweden na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia mradi wa AfroSAFE.
Amesema ajali za barabarani bado ni changamoto kubwa ya usalama wa jamii na zinasababisha vifo, majeraha, ulemavu wa kudumu pamoja na uharibifu wa miundombinu na vyombo vya usafiri, hali inayoongeza gharama za matengenezo kwa Serikali na wananchi.

Dkt. Msonde ametoa rai kwa wataalamu wa mafunzo hayo kushiriki kikamilifu ili mafunzo yawasaidie kuongeza ujuzi na utaalamu wa kihandisi katika masuala ya usalama barabarani pamoja na kubaini mapungufu yaliyopo katika miundombinu ya barabara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Ujenzi, Eng. Kashinde Mussa, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha Serikali inapunguza ajali za barabarani kwa angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.
Ameeleza kuwa takwimu za dunia zinaonesha ajali za barabarani zinaongezeka, ambapo takribani watu milioni 1.19 hupoteza maisha kila mwaka, huku kati ya milioni 20 hadi 50 wakipata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali hizo.

Amebainisha kuwa mafunzo hayo yatasaidia kupunguza makosa yanayotokana na miundombinu ya barabara, huku yakilenga kuwajengea uwezo wataalamu kutoka TANROADS na TARURA katika kubuni, kusanifu na kujenga barabara salama zaidi.
Naye, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Jackline Masaki, amesema mafunzo hayo yatawawezesha wahandisi kupata ujuzi wa kina katika ukaguzi na uchunguzi wa usalama barabarani ili kuhakikisha barabara zinakuwa salama kwa watumiaji wote.
Zaidi ya wahandisi 50 wanashiriki katika mafunzo hayo ya siku tatu.




