Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

SERIKALI imewataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kuhakikisha migogoro ya ardhi iliyopo katika maeneo yao inatatuliwa kwa wakati ili kuepusha malalamiko ya wananchi.

Onyo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Kaspar Kaspar Mmuya alipokuwa akiongea na watumishi wa sekta hiyo kutoka taasisi mbalimbali za umma Mkoani hapa.

Ameeleza kuwa ni jukumu la wataalamu wa sekta hii kuhakikisha kero na migogoro yoyote inayohusiana na masuala ya ardhi inashughulikiwa ipasavyo na kwa wakati ili wananchi wapate haki zao.

‘Ninyi ni wawakilishi wa Mheshimiwa Rais katika sekta hii, onyesheni weledi wenu, fanyeni kazi kwa uadilifu mkubwa, kuweni na maadili mema, tendeni haki kwa wananchi wote ili wawaamini, wengi wenu mnaitwa wapiga dili’, amesema.

Ameonya kuwa serikali haitamvumilia mtumishi yeyote wa sekta hii anayeendekeza vitendo vya upigaji dili badala ya kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo iliyopo.

Naibu Waziri amebainisha majukumu yao ya msingi kuwa ni kupanga matumizi bora ya ardhi, kupima maeneo husika na kuwamilikisha wananchi kwa kuwapatia hati za umiliki na sio kuficha mafaili yao na kuwapiga kalenda kila siku.

Amesisitiza kuwa uadilifu na haki ndio msingi wa utumishi bora, hivyo akawataka kubadilika kiutendaji ili jamii iendelee kuwaamini na kuwapa ushirikiano huku akiongeza kuwa migogoro mingi ya ardhi inasababishwa na wataalamu wenyewe.

Mmuya amemwagiza Kamishna wa Ardhi wa Mkoa huo na Wakuu wa Idara kumwandalia taarifa inayoonesha idadi ya migogoro iliyopo, iliyoshughulikiwa, mahali ilipo, chanzo na hatua iliyofikiwa katika utatuzi wake.

Aidha ameagiza kuwepo mfumo unaoeleweka wa utatuzi wa migogoro ya ardhi na kumtaka Kamishana wa Ardhi kulisimamia ipasavyo ili kila Mtaalamu atekeleze wajibu wake kwa kuzingatia mfumo huo na sio kufanya atakavyo.